Na Mwandishi Wetu
Wazee wa Kahama Mkoani Shinyanga wameeleza kuwa siri kubwa iliyowafanya Watanzania kuishi kwa amani kwa zaidi ya miaka 60 ni kuheshimiana, kusameheana, kuvumiliana na kutanguliza maslahi ya taifa mbele kuliko tofauti binafsi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wazee hao wamesema zamani jamii ilijengwa katika misingi ya upendo, malezi bora na utatuzi wa migogoro kwa mazungumzo badala ya mabishano au nguvu.
Mzee mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Shija mkazi Mhongolo amesema enzi zao watu walihesabiana kama ndugu bila kujali kabila, dini au eneo analotoka mtu.
“Tulikuwa tunaishi kama familia moja ukiona jirani ana shida unamsaidia, Hakukuwa na nafasi ya chuki wala ubaguzi hiyo ndiyo siri ya amani yetu,” amesema.
Mzee Shija ameeleza kuwa wazazi na walezi walikuwa mstari wa mbele kufundisha watoto maadili ya heshima, ukweli na kuwathamini wengine tangu wakiwa wadogo.
“Mtoto akilelewa vizuri hukua akiwa mtu wa amani tunapaswa kurudi kwenye malezi ya maadili ili kulinda taifa letu,” amesema.
Mzee mwingine Shabani Twaha amesema migogoro mingi ilitatuliwa kwa busara za wazee waliowakutanisha wahusika na kusikiliza pande zote kwa haki.
“Tulikaa chini, tukasikiliza kila upande na kutafuta suluhu lengo halikuwa kumwangusha mtu, bali kurudisha uhusiano mzuri,” amesema.
Wazee hao wameonya kuwa maneno ya chuki, kukosa uvumilivu na kupuuza ushauri wa wakubwa vinaweza kudhoofisha mshikamano wa jamii iwapo havitadhibitiwa mapema.
Wamesema ili kurejesha na kuimarisha siri hiyo jamii inapaswa kusikiliza wazee, kuendeleza mila nzuri za kusameheana, kutumia lugha ya staha na kujenga tabia ya kusikiliza wengine hata wanapokuwa na mawazo tofauti.
“Amani ni urithi wetu tukiilinda kwa busara na upendo, vizazi vijavyo vitaifaidi kama tulivyoifaidi sisi,” amesema mzee Twaha.
Wazee hao wamehitimisha kwa kuwataka Watanzania wote kuendelea kuwa walinzi wa umoja wa taifa, wakisisitiza kuwa amani huanza ndani ya familia ndipo huenea kwenye jamii na hatimaye hulijenga taifa imara.
#HekimaYetu #TanzaniaTulivu

No comments:
Post a Comment