Mkazi wa Kata ya Mongolo amewataka Watanzania kuendelea kulinda na kuthamini amani ya nchi, akieleza kuwa licha ya hali ya utulivu uliopo sasa, bado baadhi ya wananchi wana hofu kufuatia matukio yaliyotokea Oktoba 29.
Akizungumza kama mfugaji na mwananchi, amesema matukio hayo yameacha athari kubwa kiuchumi na kijamii, hasa kwa wafanyabiashara wadogo wakiwemo wauza mboga mboga, matunda na madereva wa bodaboda, ambao walilazimika kusitisha shughuli zao kutokana na hofu ya usalama.
Ameeleza kuwa kukosekana kwa amani kuna madhara makubwa kwa maendeleo ya taifa, ikiwemo kudorora kwa uchumi, kusimama kwa shughuli za kijamii na kupanda kwa bei za bidhaa muhimu kama mafuta na vyakula.
“Bila amani hakuna biashara, hakuna shule, wala usalama wa uhakika kwa mwananchi,” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa siasa na ushindani wa madaraka vinaweza kuwa chanzo cha migongano endapo havitasimamiwa kwa hekima, akisisitiza umuhimu wa viongozi na wananchi kukaa pamoja na kujadiliana ili kuepusha migawanyiko.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa bila kujali tofauti za kisiasa, dini au kabila, Watanzania wanapaswa kuweka mbele uzalendo na maslahi ya taifa.
“Sisi ni wamoja. Hii nchi ni yetu sote. Hatuwezi kugombania fito moja wakati tunajenga nyumba moja,” ameeleza.
Ametoa wito kwa viongozi wa dini, siasa na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kulinda amani, huku akiwahimiza wananchi kutochochewa na propaganda au kushawishiwa kufanya vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa nchi.
Ameongeza kuwa historia ya Tanzania ya zaidi ya miaka 60 ya amani ni tunu muhimu inayopaswa kuendelezwa kwa kuweka mbele upendo, mshikamano na uzalendo kama walivyofanya wazee wa zamani.
“Tusipolinda amani, tunaweza kuwapa nafasi wale wasiolitakia mema taifa letu kuleta migawanyiko na vurugu,” ameonya.
Mwisho, amewataka Watanzania wote kupenda nchi yao na kujenga mshikamano, akisisitiza kuwa amani ni msingi wa maendeleo na ustawi wa taifa.

No comments:
Post a Comment