WAKAZI WA KAHAMA WAIPONGEZA TUME YA RAIS, WASISITIZA UMOJA NA AMANI KUWA NI NGUZO YA TAIFA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 13 April 2026

WAKAZI WA KAHAMA WAIPONGEZA TUME YA RAIS, WASISITIZA UMOJA NA AMANI KUWA NI NGUZO YA TAIFA




Na Mwandishi Wetu

Wakazi wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wameeleza matumaini makubwa juu ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, wakisema hatua hiyo inaonesha dhamira ya kweli ya kujenga taifa lenye mshikamano, haki na maendeleo endelevu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao wamesema kuanzishwa kwa tume hiyo chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan ni ishara ya uongozi unaosikiliza sauti za wananchi na kutafuta suluhisho la kudumu kwa changamoto zilizojitokeza.

Mkazi wa Kahama Mjini, Bi. Rehema Juma, amesema hakuna maendeleo yanayoweza kupatikana bila amani, hivyo jitihada zozote zinazolenga kuimarisha utulivu zinapaswa kuungwa mkono na kila Mtanzania.


“Kahama ni eneo la biashara, kilimo na shughuli mbalimbali za kiuchumi hivyo ili watu wafanye kazi kwa uhuru na kujiamini, lazima kuwe na amani, Tume hii ni hatua nzuri ya kulinda hali hiyo,” amesema.

Naye Bw. Juma Masud wa Kata ya Nyasubi amesema taifa lenye watu wanaosikilizana huwa na nafasi kubwa ya kusonga mbele kwa haraka kuliko taifa lenye migogoro isiyoisha.




Wananchi hao pia wameeleza kuwa matarajio yao makubwa ni kuona mapendekezo ya tume yakisaidia kuongeza maridhiano na kuimarisha mshikamano wa Watanzania bila kujali tofauti za kisiasa, kijamii au kiitikadi.

Mkazi mwingine wa Kahama, Mama Halima Said, amesema wakati umefika kwa Watanzania kuangalia mbele na kujenga taifa moja lenye upendo na ushirikiano.


“Tofauti zipo katika kila jamii, lakini jambo la muhimu ni namna tunavyokaa pamoja na kuzitatua kwa hekima. Hapo ndipo nguvu ya taifa inapopatikana,” amesema.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso