UONGOZI WA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA IFUGANDI WANG’ARA SEKTA YA MADINI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 1 April 2026

UONGOZI WA CHAMA KIKUU CHA USHIRIKA IFUGANDI WANG’ARA SEKTA YA MADINI




Na Paul Kayanda, Geita

KATIKA kijiji cha Ifugandi, kilichopo Kata ya Busolwa, Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Chama Kikuu cha Ushirika wa Wachimbaji Madini kimeendelea kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi kupitia sekta ya madini, hususan uchimbaji wa dhahabu.

Chini ya uongozi wa Mwenyekiti Mtingwa Mihambo, kwa kushirikiana na Mjumbe wa Bodi Masanja Philipo John pamoja na wajumbe wengine, ushirika huo umefanikiwa kuwaunganisha wachimbaji wadogo na kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa mfumo wa pamoja wenye tija.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti Mihambo alisema kuwa ushirika huo umeongeza uzalishaji wa madini na kuinua kipato cha wanachama wake, jambo ambalo limechangia kuboresha maisha ya wananchi wa eneo hilo.

“ Kupitia ushirika wetu, wachimbaji wamepata sauti ya pamoja na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi katika kijiji chetu,” alisema Mihambo.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, kijiji cha Ifugandi ni miongoni mwa maeneo yanayochangia mapato ya wilaya kutokana na shughuli za uchimbaji wa dhahabu. Aidha, biashara ndogondogo zimekua kwa kasi kufuatia uwepo wa machimbo kupitia ushirika huo.

Wachimbaji wadogo katika eneo hilo wameendelea kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa ndani licha ya kukumbana na changamoto za mara kwa mara, ikiwemo uwekezaji mdogo na migogoro ya maeneo ya machimbo kati yao na wawekezaji wakubwa.

Mbali na wachimbaji, ushirika huo pia umewezesha makundi mbalimbali ya kijamii kunufaika kiuchumi, ikiwemo kuongeza ajira kwa vijana na watu wa rika tofauti. Mfano ni Christina Pius, mama lishe wa Ifugandi, ambaye ameeleza jinsi shughuli za uchimbaji zilivyoongeza wateja na kukuza biashara yake.

“Ushirika huu umetusaidia hata sisi wafanyabiashara wadogo kupata kipato cha uhakika,” alisema Pius.

Mjumbe wa Bodi, Masanja Philipo John, alisema kuwa ushirika huo pia umejikita katika kuwajengea wanachama uelewa wa sheria na taratibu za uchimbaji salama pamoja na umuhimu wa kuhifadhi mazingira ili shughuli hizo zifanyike kwa tija zaidi.

Aidha, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuyajali makundi ya vijana na kuyapa kipaumbele katika sekta ya madini, akimtaja kuwa ni “Mama wa Dhahabu”.

“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutukumbuka sisi vijana. Katika kipindi chake tumenufaika zaidi kupitia sekta ya madini. Leo hii tunamiliki leseni za uchimbaji. Tunawahimiza vijana kuacha kukaa vijiweni na badala yake wajikite katika shughuli za uzalishaji,” alisema.

Pamoja na mafanikio hayo, viongozi hao wameeleza kuwa bado wanakabiliana na changamoto mbalimbali, zikiwemo miundombinu duni na migogoro ya mara kwa mara katika maeneo ya machimbo. Hata hivyo, wameahidi kuendelea kushirikiana na serikali pamoja na wadau wengine ili kuboresha sekta hiyo.

Uongozi wa Chama cha Ushirika Ifugandi umeendelea kuwa mfano wa mafanikio katika kuwawezesha wachimbaji wadogo na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Wilaya ya Nyang’hwale na Mkoa wa Geita kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso