Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, akizungumza katika hafla ya kukabidhi jengo la ofisi ya Polisi Jamii pamoja na ofisi ya Operesheni na Mafunzo Wilaya ya Kahama, lililogharimu takribani shilingi milioni 25.Neema Nkumbi Kahama
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amepongeza ushirikiano mkubwa kati ya wananchi, viongozi na wadau uliofanikisha ujenzi wa ofisi ya Polisi Jamii pamoja na ofisi ya Operesheni na Mafunzo Wilaya ya Kahama, lililogharimu takribani shilingi milioni 25.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi jengo hilo, Magomi amesema mradi huo ni matokeo ya dhana ya ulinzi shirikishi, ambapo wananchi wamekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani na usalama.
“Ni jambo la kujivunia kuona wananchi wanajitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha wanapata huduma bora za usalama, Huu ni mfano mzuri wa ulinzi shirikishi,” amesema Magomi.
Kwa upande wake, Mkuu wa kituo cha polisi Wilaya ya Kahama OCD Mtaju Mayombo akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo hilo amesema ulianza mwezi Mei mwaka jana na kukamilika Desemba, likiwa na huduma zote muhimu ikiwemo maji, umeme na samani za ofisi.
Ameeleza kuwa jengo hilo lina ofisi za Polisi Jamii pamoja na ofisi ya Operesheni, hatua itakayosaidia kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi.
Diwani wa Kata ya Kahama Mjini, Godson Andrew, amesema ushirikiano uliopo kati ya wananchi na Jeshi la Polisi umeifanya Kahama kuendelea kuwa salama, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kushiriki katika shughuli za maendeleo na masuala ya ulinzi.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Kahama, Charles Machali, amesema wafanyabiashara wana uhusiano mzuri na Jeshi la Polisi, akibainisha kuwa askari wamekuwa wakitoa huduma kwa haraka pindi wanapohitajika, jambo linalosaidia kulinda mali zao na kukuza biashara.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Makampuni ya Ulinzi Kahama, Fabian Marius, amesema makampuni ya ulinzi binafsi yamekuwa yakishirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi, na kuomba kuendelea kwa mafunzo kwa askari wao ili kuongeza weledi,Pia ameomba kudhibiti makampuni yasiyo rasmi yanayoharibu ushindani wa haki katika sekta hiyo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limeahidi kuendelea kushirikiana na wananchi ili kuhakikisha mazingira ya Kahama yanaendelea kuwa salama na yenye utulivu.















No comments:
Post a Comment