
Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza mkakati wa haraka wa mambo sita yenye lengo la kuirejesha Tanzania kwenye misingi yake ya amani, ukiwa ni muendelezo wa falsafa yake ya 4R.
Katika hatua ya kwanza ya kusafisha kidonda cha machafuko ya Oktoba 2025, Rais ametangaza kuunda Tume ya Maridhiano itakayowashirikisha wadau wote muhimu nchini.
Rais alibainisha kuwa ghasia hizo zilichelewesha mpango wake wa awali wa maridhiano, hivyo sasa atabadili hadidu za rejea ili kuendana na mazingira ya sasa ya kidemokrasia na kijamii, akilenga kuziba mianya ya mgawanyiko miongoni mwa Watanzania.
Kwenye upande wa haki na sheria, Rais ametoa amri ya kuundwa kwa chombo maalum cha upelelezi kitakachoshughulikia viashiria vyote vya jinai vilivyotajwa kwenye ripoti ya tume.
Chombo hicho kimepewa jukumu zito la kuchunguza vifo vya watoto, kushughulikia madai ya miili ambayo haijapatikana, na kufuatilia hatma ya watu wanaodaiwa kutekwa.
Hatua hii inaenda sambamba na uamuzi wa kibinadamu ambapo serikali imejitolea kugharamia matibabu, vifaa saidizi, na viungo bandia kwa majeruhi wote, huku ikiahidi kutoa "mkono wa faraja" kwa wafanyabiashara wadogo waliopoteza mitaji yao na ambao hawakuwa na bima ya kulinda biashara zao.
Aidha Rais Samia aliitaka jamii kusimama na maneno ya Mungu, na kuwaomba viongozi wa dini na wananchi kwa ujumla kuliombea taifa lipate uponyaji wa kiroho na kisaikolojia.
Alisisitiza kuwa ingawa ni rahisi kubomoa nchi, ni vigumu sana kuijenga upya, hivyo akatoa wito kwa kila Mtanzania kulinda amani na kuepuka kushawishiwa na watu wenye nia ya kuvuruga nchi.
Rais ameweka wazi kuwa Tanzania itaendelea kujenga mfumo wake wa demokrasia kwa kuzingatia mila, desturi, na mchakato wake wa ndani, huku akiwaonya watumishi wa umma kuhusu uwajibikaji, maadili, na matumizi mabaya ya rasilimali ambayo mara nyingi ndiyo huchochea kutoridhika kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment