KAHAMA: MKUU WA WILAYA AAGIZA ULIPAJI WA MADENI, WAFANYABIASHARA 750 WADAIWA SOKO LA NAMANGA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 28 April 2026

KAHAMA: MKUU WA WILAYA AAGIZA ULIPAJI WA MADENI, WAFANYABIASHARA 750 WADAIWA SOKO LA NAMANGA


Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, akizungumza na wafanyabiashara wa Soko la Namanga lililopo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga 

Neema Nkumbi, Kahama

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, ameagiza wafanyabiashara zaidi ya 750 wa Soko la Namanga lililopo Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga kulipa madeni yao ya mapato ya serikali, yanayodaiwa tangu mwaka 2020.

Wafanyabiashara hao, wanaofanya biashara juu ya meza ndani ya soko hilo, wanadaiwa Shilingi 10,000 kwa mwezi kila mmoja, hali iliyosababisha Halmashauri kukosa mapato ya zaidi ya Shilingi milioni 450 katika kipindi cha miaka mitano.

Akizungumza katika mkutano wa kusikiliza na kutatua kero za wafanyabiashara hao, Nkinda amesema hali ya kutolipa mapato imekuwa kikwazo kikubwa cha maboresho ya miundombinu ya soko hilo.

“Ni ukweli usiopingika kwamba soko hili linahitaji maboresho, lakini haiwezekani kuboresha wakati hamlipi mapato. Chanzo cha maboresho ya soko letu ni sisi wenyewe,” amesema Nkinda.

Ameongeza kuwa zaidi ya wafanyabiashara 750 hawajalipa mapato tangu mwaka 2020, akisisitiza kuwa ni lazima kila mmoja awajibike ili kubadili taswira ya soko hilo.

Kwa upande wake, Mhasibu wa Mapato wa Manispaa ya Kahama, Eliot Kalulu, amesema madeni hayo yamekuwa yakiongezeka kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kushindwa kulipa kwa wakati, hali iliyosababisha mzigo wa deni kuwa mkubwa.

Wakizungumza katika mkutano huo, baadhi ya wafanyabiashara walilalamikia ubovu wa miundombinu ya soko, wakisema inasababisha hasara kutokana na magari ya mizigo kushindwa kuingia ndani ya soko.

Hapiness John ameiomba halmashauri kuwaongezea muda wa kulipa madeni yao pia waruhusiwe kulipa kidogo kidogo kwani madeni ni makubwa ambayo yanawashinda kulipa kwa mara moja.


“Sisi hatukatai kulipa, lakini muda uliotolewa ni mfupi na mazingira ya biashara yanatubana,” amesema.

Jonas Moses, mfanyabiashara wa viazi, amesema ubovu wa barabara ndani ya soko zinawalazimu kuongeza gharama za usafirishaji wa bidhaa.

Naye Barnaba Paulo amesema baadhi ya wafanyabiashara wamerithi madeni ya waliotangulia, hivyo akaomba Halmashauri kuangalia upya utaratibu wa adhabu.

Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Flora Sangiwa, alisema Halmashauri imeongeza muda wa ulipaji wa madeni hayo kutoka Aprili 30 hadi Mei 30 mwaka huu ili kutoa nafasi kwa wafanyabiashara kulipa.



MWISHO.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso