JOSEPH YUSUFU: AMANI NI NGAO YA UCHUMI NA MAISHA YA WANANCHI KAHAMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 17 April 2026

JOSEPH YUSUFU: AMANI NI NGAO YA UCHUMI NA MAISHA YA WANANCHI KAHAMA




Na Mwandishi Wetu

Baadhi ya wakazi wa Kahama mkoani Shinyanga wameitaka jamii kuendelea kulinda amani na utulivu wa nchi, wakisema vurugu na machafuko yana madhara makubwa kwa wananchi hasa wenye kipato cha chini wanaotegemea kazi za kila siku kujikimu.

Akizungumza kuhusu hali ya kijamii na kiuchumi baada ya matukio yaliyopita, mkazi wa Kahama, Joseph Yusufu, amesema matokeo ya machafuko hayo hayapaswi kujirudia kwani huathiri maisha ya watu wengi pamoja na shughuli za uzalishaji na biashara.

Amesema wananchi wa kawaida ndio wanaobeba mzigo mkubwa wa matukio hayo kwa kuwa wengi wao hutegemea kutoka kila siku kutafuta kipato cha kuendesha maisha yao.

“Wananchi wengi ni wa maisha ya chini, Inapotokea hali ya vurugu au kufungwa kwa shughuli za kila siku hata kwa siku chache tu, maisha yanakuwa magumu kwa sababu watu wanategemea kufanya kazi ndipo wapate chakula,” amesema Joseph.

Aidha, ameiomba Serikali kuendelea kusikiliza wananchi na kuboresha maeneo yenye changamoto ili kuimarisha zaidi amani iliyopo na kurejesha hali ya kawaida kwa wananchi wakati wowote panapotokea sintofahamu.

Kwa upande wa biashara, amesema machafuko husababisha hasara mbalimbali ikiwemo kusimama kwa shughuli za kiuchumi na uharibifu wa mali za wananchi, jambo linalowaumiza wengi.

Kuhusu vijana wanaoshawishika kujiunga na makundi yanayoweza kusababisha migogoro, Joseph amewataka kutafakari kwa kina madhara na faida ya kila jambo kabla ya kushiriki.

“Vijana ni nguvu kazi ya taifa na msingi wa familia nyingi, Ni muhimu kuchagua njia sahihi na kuachana na makundi yasiyo na tija ambayo yanaweza kuharibu maisha yao na ya wengine,” amesema.

Ameongeza kuwa vijana wanapaswa kuelekeza nguvu zao katika shughuli za maendeleo, elimu na ubunifu badala ya kushiriki vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na ustawi wa taifa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso