COMPASSION KAHAMA YAANZISHA MTAALA WA ALPHA KUPAMBANA NA WATOTO WA MTAANI NA KUWAKUZA KIROHO VIJANA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 20 April 2026

COMPASSION KAHAMA YAANZISHA MTAALA WA ALPHA KUPAMBANA NA WATOTO WA MTAANI NA KUWAKUZA KIROHO VIJANA


Huduma ya maendeleo ya ukuaji wa mtoto na kijana ya Compassion Cluster Kahama imeanzisha mtaala maalumu wa Alpha unaolenga kuwasaidia vijana wanaoishi katika mazingira magumu pamoja na kuwaongoza kumjua Yesu, hatua inayotajwa kusaidia kupunguza tatizo la watoto wa mitaani katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mtaala huo uliofanyika katika Kanisa la Africa Inland Church Tanzania (AICT) Kahama Mjini, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amekiri kuwepo kwa changamoto ya watoto wa mitaani katika manispaa hiyo.


Amesema ili kutokomeza tatizo hilo, wazazi na walezi wanapaswa kusimamia wajibu wao wa malezi na kuhakikisha watoto wanapata uangalizi unaostahili tangu wakiwa wadogo.


Kwa upande wa Compassion, mmoja wa maofisa wa shirika hilo amesema zaidi ya vijana laki moja wanahudumiwa na taasisi hiyo nchini Tanzania, huku takribani vijana 3,500 wakihudumiwa katika Mkoa wa Shinyanga.


Amesema vijana hao hupatiwa huduma mbalimbali za msingi zikiwemo elimu, malazi, mavazi pamoja na malezi yanayowajengea maisha bora ya baadaye.


Awali akisoma risala kwa mgeni rasmi, mmoja wa vijana wa huduma hiyo, Happyness Daniel, amesema lengo la mtaala wa Alpha ni kuwakutanisha vijana na kuwasaidia wale wanaovutwa na mambo ya dunia kurejea katika misingi ya maadili mema.


Amesema kupitia mpango huo, vijana watapatiwa mwongozo sahihi na kulelewa katika maadili yatakayowasaidia kuwa raia wema na wenye hofu ya Mungu.


Naye Fatanly John amesema mtaala huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa kwa vijana kwani utawapa nafasi ya kujifunza mambo muhimu kama mafundisho ya Biblia, ukarimu, kuheshimiana na umuhimu wa kuishi kwa upendo bila kujali umri au hali za mtu.


Kwa upande wao, Stephania Gabriel na Lucy Macheyeke wamesema malezi ya mtoto huanza tangu hatua za awali kabisa na yanahitaji ushirikiano wa wazazi wote wawili, baba na mama.


Wamesisitiza kuwa msingi wa maadili ya mtoto hutegemea namna wazazi walivyolelewa na jinsi wanavyoishi, hivyo jamii inapaswa kuwekeza zaidi katika malezi bora ya watoto ili kujenga kizazi chenye maadili na uwajibikaji.








Na Mwandishi Wetu

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso