Watu wenye ulemavu Wilaya ya Kahama wameiomba Serikali kuboresha mazingira na miundombinu katika taasisi mbalimbali za kijamii ili waweze kupata huduma kwa usawa sawa na watu wasio na ulemavu.
Ombi hilo limetolewa wakati wa ziara ya Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Ndugu Rabia Abdallah Hamid, iliyofanyika jana katika Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Akiwasilisha taarifa ya Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) Wilaya ya Kahama, Katibu wa shirikisho hilo, Charles Kafuku, amesema watu wenye ulemavu wanakumbana na changamoto kubwa katika upatikanaji wa huduma muhimu kwenye taasisi mbalimbali za kijamii.
Amezitaja baadhi ya taasisi hizo kuwa ni hospitali, vituo vya polisi, halmashauri na mahakama, akibainisha kuwa miundombinu iliyopo mara nyingi haizingatii mahitaji yao. Aidha, amesema baadhi ya majengo ya serikali na binafsi hayana mazingira rafiki yanayowezesha watu wenye ulemavu kupata huduma kwa urahisi.
Kafuku ameongeza kuwa wanawake wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto zaidi wanapohitaji huduma za afya, hususan wakati wa kujifungua. Ameeleza kuwa ukosefu wa vifaa maalum, vitanda vinavyofaa pamoja na changamoto ya usiri katika utoaji wa huduma hizo ni miongoni mwa masuala yanayohitaji kufanyiwa kazi haraka.
Katika hatua nyingine, wachimbaji wadogo wa madini wameiomba Serikali kutatua changamoto zao kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na mwakilishi wa vijana wachimbaji madini Kahama, Simon Mgali. Mgali amependekeza kuwepo kwa utaratibu wa utoaji wa mikopo ya vifaa badala ya fedha taslimu kupitia vikundi, hasa kwa wachimbaji wadogo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Khamis Mnubi, Afisa Maendeleo wa manispaa hiyo amesema ni muhimu kwa wanufaika wa mikopo kuzingatia masharti yaliyowekwa ili kuhakikisha uendelevu wa mifuko ya uwezeshaji.
Kwa upande wake, Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (SUKI), Rabia Abdallah Hamid, amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeongeza ushirikishwaji wa makundi mbalimbali ya kijamii, ikiwemo watu wenye ulemavu, vijana, wafanyakazi na asasi zisizo za kiserikali (NGOs), ili kurahisisha utoaji wa maoni na mapendekezo.
Amesisitiza kuwa taarifa iliyowasilishwa itapelekwa katika ngazi husika kama ilivyo, bila kufanyiwa mabadiliko, ili kuhakikisha sauti za wananchi zinasikika na kuzingatiwa katika maamuzi ya maendeleo.
“Hoja zilizowasilishwa zina mashiko na zinalenga kuboresha sera na sheria kwa manufaa ya jamii kwa ujumla. Nawaahidi nitaibeba kama ilivyo,” amesema Rabia.













No comments:
Post a Comment