UMEME WA UHAKIKA WACHOCHEA MAPINDUZI YA UZALISHAJI DHAHABU - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 28 March 2026

UMEME WA UHAKIKA WACHOCHEA MAPINDUZI YA UZALISHAJI DHAHABU




Na Mwandishi Wetu, Geita

MENEJA Mkuu wa Kiwanda cha Kuchenjulia Dhahabu (CIP) kilichopo wilayani Nyang’hwale mkoani Geita, Ali Mudeme, ameeleza mafanikio makubwa ya uzalishaji wa dhahabu yanayotokana na matumizi ya mitambo ya kisasa, akibainisha kuwa hatua hiyo imeongeza tija kwa kiwango kikubwa.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari waliotembelea kiwanda hicho, Mudeme alisema uwekezaji katika teknolojia ya kisasa ya uchakataji dhahabu umewezesha kuongezeka kwa uzalishaji pamoja na ubora wa madini yanayozalishwa.

Alifafanua kuwa kiwanda hicho kimekuwa chachu ya maendeleo kwa wakazi wa eneo hilo kwa kutoa ajira kwa wazawa na kuchochea shughuli nyingine za kiuchumi.

“Kwa sasa tunajivunia kuona kuwa kiwanda chetu kinachangia kwa kiasi kikubwa katika mapato ya Serikali kupitia ukusanyaji wa maduhuli mbalimbali yatokanayo na shughuli za madini,” alisema Mudeme.

Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kuboresha sekta ya nishati ya umeme nchini, hususan katika maeneo ya migodi.

Alisema upatikanaji wa umeme wa uhakika umeongeza ufanisi wa mitambo ya CIP, hali iliyochochea ongezeko la uzalishaji wa dhahabu.

Mudeme alisisitiza kuwa maboresho hayo ya nishati yamekuwa kichocheo kikubwa kwa wawekezaji na wadau wa sekta ya madini, akiongeza kuwa bila umeme wa uhakika, uzalishaji usingefikia kiwango cha sasa.

Hata hivyo, aliiomba Wizara ya Nishati kuendelea kuimarisha miundombinu ya umeme, hasa katika kipindi cha mvua za masika, ili kuepusha changamoto za kukatika kwa umeme ambazo zinaweza kuathiri uzalishaji.

Kwa upande wao, waandishi wa habari George Maziku, Mohab Dominick pamoja na Patrick Mabula walipata fursa ya kujionea namna mitambo ya kisasa inavyofanya kazi katika uchakataji wa dhahabu, jambo lililowaongezea uelewa kuhusu mchango wa viwanda vya CIP katika kukuza uchumi wa taifa.

“Kwa niaba ya waandishi wa habari tuliofika hapa, tumejionea wenyewe kiwango cha juu cha utendaji kazi kupitia teknolojia ya kisasa ya mitambo. Hii ni hatua muhimu itakayosaidia Serikali kuongeza mapato na kunufaisha Watanzania wanaozunguka maeneo ya uwekezaji,” alisema George Maziku, mwandishi wa habari kutoka Gazeti la Rada.

Kwa ujumla, ziara hiyo imeonyesha wazi namna sekta ya madini inavyoendelea kuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya Tanzania, huku ushirikiano kati ya Serikali na wadau wa sekta hiyo ukiendelea kuzaa matokeo chanya.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso