Neema Nkumbi, Ushetu
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amewahimiza wanawake kujitambua, kujithamini na kujiona kuwa na nafasi ya juu katika jamii ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
Akizungumza leo machi 8, 2026 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kimkoa katika Halmashauri ya Ushetu, Wilaya ya Kahama, Mhe. Mhita amesema mwanamke anapaswa kujiona wa thamani kubwa kwani namna anavyojichukulia ndivyo jamii itakavyomchukulia.
Akizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu inayohusiana na kufikia Dira ya Taifa 2050, amesema Tanzania inalenga kuwa na uchumi imara, jamii yenye ustawi na wananchi wenye maisha bora, hivyo uwekezaji kwa wanawake na wasichana ni jambo muhimu katika kufikia malengo hayo.
Amesema mwanamke akielimika familia inaelimika, na akipewa fursa za kiuchumi jamii kwa ujumla hunufaika, Aidha amesisitiza kuwa ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi husaidia kufanya maamuzi kuwa jumuishi na yenye manufaa kwa watu wote.
“Duniani mtu atakuchukulia vile ambavyo wewe unamchukulia na vile utakavyojichukulia ndivyo utakavyojiweka, Mwanamke hapaswi kujiona wa daraja la chini au la kati bali ajione wa daraja la juu,” amesema Mhita.
Ameongeza kuwa serikali imeendelea kuboresha sheria na miongozo mbalimbali ili kuondoa vikwazo vilivyokuwa vinawakandamiza wanawake na kuweka mazingira bora ya usawa katika nafasi za maamuzi na uongozi.
Akitolea mfano uwepo wa miongozo inayotaka katika bodi zenye wajumbe saba angalau watatu wawe wanawake, hatua inayolenga kuongeza uwakilishi wa wanawake katika ngazi mbalimbali za uongozi.
Aidha amewataka wazazi na walimu kuhakikisha watoto wa kike wanapata fursa ya elimu ili kuwaandaa kuwa viongozi wa baadaye na wadau muhimu katika maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake, Afisa kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA), Angel Mwaipopo, amesema mamlaka hiyo inaendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha wananchi, hususan wanawake na wasichana, wanapata huduma ya maji safi na salama kwa urahisi.
Ameeleza kuwa upatikanaji wa maji kwa muda wote ni moja ya hatua muhimu ya kupunguza mzigo kwa wanawake ambao mara nyingi hubeba jukumu la kutafuta maji kwa ajili ya familia.
Maadhimisho hayo ya Siku ya Wanawake Duniani kwa Mkoa wa Shinyanga yamefanyika katika Halmashauri ya Ushetu yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Haki kwa Wanawake na Wasichana: Msingi wa Maendeleo Jumuishi Kufikia Dira ya 2050.”






















No comments:
Post a Comment