QATAR YAINGIA KWENYE ORODHA YA MATAIFA 11 YANAYOKULA MBUZI WA TANZANIA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 21 March 2026

QATAR YAINGIA KWENYE ORODHA YA MATAIFA 11 YANAYOKULA MBUZI WA TANZANIA




Katika kile kinachoonekana kama ushindi wa diplomasia ya kiuchumi na ubora wa bidhaa za Tanzania, nchi ya Qatar imetangaza rasmi kufungua soko la nyama ya mbuzi na kondoo kutoka Tanzania.


Hatua hiyo iliyopokelewa kwa shangwe na wadau wa mifugo, imekuja baada ya nchi hiyo kujiridhisha na hatua madhubuti zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kudhibiti magonjwa ya mifugo na kuimarisha viwango vya usalama wa chakula vinavyokubalika kimataifa.



Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk. Benezeth Lutege, amethibitisha kuwa Qatar imetoa ruhusa hiyo Machi 17, 2026, baada ya kuridhishwa na ujenzi wa karantini za kisasa pamoja na kampeni kabambe ya chanjo ya mifugo nchini.

Awali, soko hilo lilifungwa tangu Agosti 25 mwaka jana kutokana na hofu ya ugonjwa wa midomo na miguu, lakini jitihada za serikali kueleza ukweli wa kitaalamu na kuimarisha maabara za TVLA zimesaidia kurejesha imani ya soko hilo muhimu duniani.

Kurejea kwa soko la Qatar kuna maana kubwa kiuchumi kwani nchi hiyo imekuwa ikipokea wastani wa tani 3,000 za nyama kutoka Tanzania. Kwa kuzingatia kuwa nyama ya mbuzi pekee inachangia asilimia 64.69 ya mauzo yote ya nyama nje ya nchi, kufunguliwa huku ni kichocheo kikubwa cha kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia Aprili mwaka jana, Tanzania ilikuwa imevuna dola za Marekani milioni 44.07 kutokana na mauzo ya nyama nje, na sasa kurejea kwa Qatar kutaongeza kasi ya kufikia malengo makubwa zaidi ya kibiashara.

Kijamii na kiajira, hatua hii ni neema ya moja kwa moja kwa mfugaji wa vijijini. Kuongezeka kwa mahitaji ya nyama ya mbuzi na kondoo katika nchi 11 ambazo Tanzania inauza sasa, ikiwemo Saudi Arabia, UAE, na Vietnam, kunamaanisha kuwa bei ya mifugo itaimarika na soko litakuwa la uhakika. Hii inatoa motisha kwa vijana kuwekeza katika ufugaji wa kisasa na machinjio kufuata vigezo vya kimataifa, jambo ambalo linaendana na dira ya serikali ya kubadili sekta ya mifugo kuwa biashara yenye tija badala ya sifa pekee.

Aidha, sharti la Qatar la kutaka kila mzigo uthibitishwe na Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) ni fursa ya kuonyesha ulimwengu kuwa bidhaa za Tanzania ni salama na zenye ubora.

Kwa kufanya hivi, serikali haitafuti tu masoko, bali inajenga chapa (brand) ya nyama ya Tanzania inayoweza kushindana na mataifa mengine makubwa. Ni wazi kuwa sasa mpira upo kwa wafugaji na wasindikaji wa nyama kuhakikisha wanatunza sifa hii ili kutanua wigo wa soko letu kote ulimwenguni.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso