Na Paul Kayanda, Kahama
Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini, Benjamin Lukubha Ngayiwa, Machi 15, 2026 ameandaa futari maalum iliyowakutanisha waumini wa dini ya Kiislamu pamoja na wananchi mbalimbali wa jimbo hilo.
Futari hiyo imefanyika katika mazingira ya upendo, mshikamano na kuheshimiana kati ya wananchi na Mbunge wao, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mahusiano ndani ya jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Sheikh wa Wilaya ya Kahama, Omary Damka, alimpongeza Mbunge Ngayiwa kwa moyo wa kujali na kuwakumbuka waumini wa Kiislamu katika kipindi hiki kitukufu cha Mwezi wa Ramadhani.
Alisema kitendo hicho kinaonesha mshikamano na upendo kwa wananchi bila kujali tofauti za dini au mitazamo ya kisiasa.
Sheikh Damka pia aliwakumbusha waumini wa Kiislamu umuhimu wa kudumisha mahusiano mema katika jamii kwa kuendelea kuheshimiana, kusaidiana na kuishi kwa amani na upendo wakati wote.
Wananchi waliohudhuria futari hiyo walionesha furaha na shukrani zao kwa Mbunge Ngayiwa kwa kuandaa tukio hilo, wakisema limeimarisha umoja na mshikamano katika jamii ya Kahama.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mbunge Ngayiwa alisema lengo la kuandaa futari hiyo ni kuwakutanisha wananchi wa makundi mbalimbali, wakiwemo wenye dini na wasio na dini, ili kupata fursa ya kukutana na kubadilishana mawazo kama familia moja.
Alisema kama Mbunge wa Jimbo la Kahama Mjini ana jukumu la kuwatumikia wananchi wote bila ubaguzi, hivyo matukio kama hayo husaidia kuimarisha umoja na mshikamano katika jamii.
Kwa ujumla, futari hiyo imekuwa ishara ya mshikamano wa kijamii na kuthibitisha kuwa upendo na ushirikiano vina nafasi kubwa katika kujenga jamii yenye amani na maendeleo.








No comments:
Post a Comment