MARIDHIANO DAY: BUTIKU, MAKINDA NA VIONGOZI WA DINI WAHIMIZA UMOJA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 5 March 2026

MARIDHIANO DAY: BUTIKU, MAKINDA NA VIONGOZI WA DINI WAHIMIZA UMOJA



KATIKA kile kinachoonekana ni harakati za makusudi za kuponya majeraha ya kisiasa na kijamii nchini, viongozi waandamizi na wastaafu wametoa wito mzito kwa Watanzania kuukubali uhalisia wa uongozi uliopo na kuzika chuki ambazo zimekuwa zikichelewesha maendeleo ya Taifa.

Akizungumza Machi 4, 2026, katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Maridhiano (Maridhiano Day) mkoani Mwanza, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Mzee Joseph Butiku, amewataka wananchi kuacha kutaabika na mawazo ya kutoitambua mamlaka, badala yake wakubali kuwa nchi ina Rais aliyejipambanua kwa vitendo katika kurejesha umoja.

“Tukubali uhalisia kuwa nchi tayari ina Rais aliye tayari kwa maridhiano. Tume aliyoiunda imezidishiwa muda hadi Aprili, hivyo tuwe na subira, tusubiri aje atuambie jambo litakalotusaidia kwenye mazungumzo yetu,” alisema Mzee Butiku, akisisitiza kuwa amani ya kweli haiwezi kupatikana bila haki.

Naye Spika mstaafu, Anne Makinda, amegusia hitaji la vijana kubadili mtazamo, akionya kuwa chuki na malumbano yasiyo na tija kwenye mitandao ya kijamii ni adui wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050. Alihimiza vijana kutumia nguvu zao kwenye kazi halali za kipato badala ya kupoteza muda mwingi kwenye simu, jambo ambalo ndilo msingi wa uzalendo wa kweli.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), Sheikh Alhad Mussa Salum, alitoa ujumbe wa kugusa hisia akumbushe kuwa kuzaliwa Tanzania ni undugu wa damu unaopaswa kulindwa kwa wivu mkubwa.

“Uzalendo ni kuwa na utayari wa kuifia nchi yako. Sheria za dini zimeletwa kulinda amani, mali, na utu. Tuishi sheria hizi ili tuwe walinzi wa Taifa letu kwa sababu hatuna nchi nyingine zaidi ya hii,” alisema Sheikh Alhad.

Harakati hizo za maridhiano zimevuka mipaka ya majukwaa makubwa na kufika hadi ngazi ya majimbo. Mbunge wa Welezo, Mhe. Asma Mwinyi, amefanya ziara ya kihistoria katika maskani za chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, akisisitiza kuwa siasa za chuki ni sumu inayobomoa utu.

“Ukatili na chuki si utamaduni wetu. Nimefika hapa kuweka siasa pembeni na kuimarisha misingi ya upendo. Tunajenga Welezo mpya na Tanzania imara kwa kusikilizana, siyo kwa kupigana vijembe,” alisema Mhe. Asma.

Ili kuhakikisha moto huu wa maridhiano hauzimiki, Katibu Mkuu wa JMAT, Dkt. Israel Ole Gabriel Maasa, ameiomba serikali kutenga ofisi maalum katika kila mkoa zitakazoratibu masuala ya amani na maridhiano, huku mgeni rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda (aliyemwakilisha Rais Samia), akipongeza juhudi hizo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso