KISWAHILI NI AJIRA: SERIKALI KUSHAWISHI META KUKIPANDISHA THAMANI KIDIJITALI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 25 March 2026

KISWAHILI NI AJIRA: SERIKALI KUSHAWISHI META KUKIPANDISHA THAMANI KIDIJITALI



Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imechukua hatua ya kihistoria katika kuhakikisha lugha ya Kiswahili inakuwa chemchemi ya ajira na kipato kwa vijana kupitia majukwaa ya kidijitali duniani.


Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amebainisha kuwa serikali imeanza mazungumzo rasmi na kampuni ya Meta, inayomiliki majukwaa ya Facebook, Instagram na WhatsApp, pamoja na Shirika la UNESCO ili kuhakikisha Kiswahili kinatambuliwa rasmi katika mifumo ya kibiashara ya mitandao hiyo.


Hatua hii inalenga kuondoa changamoto ya malipo madogo wanayopata watengeneza maudhui wa Kiswahili hivi sasa, ikilinganishwa na lugha nyingine kubwa duniani, na hivyo kufungua milango ya utajiri kwa wabunifu wa ndani.


Katika ufunguzi wa Kongamano la Tano la Idhaa za Kiswahili Duniani lililoanza jijini Arusha, imeelezwa kuwa kutambuliwa kwa Kiswahili kwenye majukwaa ya kidijitali kutaongeza thamani ya maudhui yanayozalishwa na Watanzania na kupanua wigo wa soko la watumiaji duniani kote.


Waziri Makonda amesisitiza kuwa mazingira bora ya malipo yatawawezesha vijana wanaojishughulisha na sanaa, habari, na ubunifu wa kidijitali kunufaika moja kwa moja na jasho lao.


Hii ni sehemu ya mkakati mpana wa serikali uliowezesha kufunguliwa kwa vituo 20 vya ufundishaji Kiswahili nje ya nchi kupitia balozi za Tanzania, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka vituo viwili tu vilivyokuwepo miaka mitano iliyopita.


Naye Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, akifungua kongamano hilo lenye kaulimbiu ya ‘Teknolojia ya Habari, Msingi wa Maendeleo ya Kiswahili Duniani’, amewataka waandaaji wa maudhui kutumia lugha sanifu na kuzingatia maadili ya Kitanzania.


Kwa upande wake, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Dkt. Riziki Pembe Juma, amehimiza umuhimu wa uwekezaji katika tafiti na matumizi ya Akili Unde (AI) ili kukifanya Kiswahili kiendane na mabadiliko ya sasa ya kiteknolojia.


Mbali na fursa za kiuchumi, viongozi hao wamesisitiza kuwa Kiswahili lazima kibaki kuwa chombo cha kuhamasisha amani, mshikamano na utulivu wa nchi, kwani bila amani hakuna maendeleo ya kiuchumi yanayoweza kufikiwa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso