FURSA ZA TANZANIA KATIKA CHANGAMOTO ZA VITA MASHARIKI YA KATI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 30 March 2026

FURSA ZA TANZANIA KATIKA CHANGAMOTO ZA VITA MASHARIKI YA KATI


Wakati uchumi wa dunia ukisumbuliwa na misukosuko ya kisiasa na kijeshi katika ukanda wa Mashariki ya Kati, Tanzania imetajwa kuwa na nafasi ya kipekee ya kugeuza changamoto hizo kuwa fursa za kuimarisha ukuaji wa uchumi na kuvutia mitaji mikubwa ya kigeni.


Hayo yamebainishwa na wataalamu wa sekta binafsi na uwekezaji katika mjadala maalum ulioratibiwa na kampuni ya kisheria ya ALN Tanzania kwa kushirikiana na Bankable, uliojadili mwelekeo wa uchumi wa dunia na nafasi ya kibiashara ya Tanzania kwa mwaka 2026.


Wataalamu hao wameelezea kuwa, huku migogoro ya Mashariki ya Kati ikivuruga minyororo ya ugavi na kupandisha bei ya mafuta kwa takribani asilimia 20, Tanzania inabaki kuwa "eneo salama" (Safe Haven) kutokana na utulivu wake wa kisiasa na nafasi yake ya kimkakati katika mwambao wa Bahari ya Hindi.


Mkurugenzi wa ALN Tanzania, Ed Williams, amebainisha kuwa ingawa mazingira ya uwekezaji duniani yamezidi kuwa magumu na yenye vihatarishi vingi, wawekezaji wa kimataifa sasa wanatafuta masoko yenye sera zinazotabirika na miundombinu imara ya usafirishaji, maeneo ambayo Tanzania imepiga hatua kubwa.


Mjadala huo umeibua hoja kuwa kuimarika kwa miundombinu nchini, ikiwemo reli na bandari, kunaifanya Tanzania kuwa lango kuu la biashara kwa nchi za maziwa makuu, jambo linaloweza kufidia gharama kubwa za usafirishaji wa kimataifa zilizosababishwa na kuvurugika kwa njia za bahari kufuatia migogoro hiyo ya kimataifa.


Licha ya kupanda kwa gharama za biashara duniani, wataalamu hao wamesisitiza kuwa mabadiliko haya ya kijiopolitika yanaweza kuifanya Tanzania kuwa kituo mbadala cha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, hivyo kukuza ajira na mapato ya fedha za kigeni.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso