SERIKALI imetoa onyo kali kwa wamiliki wa viwanda mkoani Pwani wanaokiuka sheria za kazi, ikisisitiza kuwa maendeleo ya kweli ya viwanda hayawezi kupatikana bila kulinda utu, afya, na maslahi ya mfanyakazi wa Kitanzania.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Mhe. Rahma Kisuo, wakati wa ziara yake ya kushtukiza wilayani Kibaha iliyolenga kukagua utekelezaji wa sheria za usalama mahali pa kazi.
Akizungumza baada ya kutembelea kiwanda cha kuunganisha magari cha GF Vehicle Assemblies Ltd na vinginevyo, Mhe. Kisuo amebainisha kuwa pamoja na uwekezaji mkubwa uliopo, bado kuna dosari zinazoumiza nguvu kazi ya Taifa, ikiwemo wafanyakazi kufanya kazi bila mikataba ya ajira.
“Hatuwezi kuwa na uzalishaji wenye tija ikiwa mfanyakazi hana uhakika wa ajira yake au anafanya kazi katika mazingira yanayohatarisha afya yake. Lazima viwanda viboreshe maslahi na mazingira ya kazi ili kuwa na maendeleo endelevu,” alisema Mhe. Kisuo.
Katika ziara hiyo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, aliweka wazi baadhi ya madudu yaliyobainika, ikiwemo wafanyakazi kulazimika kufanya kazi kwenye joto kali, vumbi la makaa ya mawe, na ukosefu wa vifaa kinga (PPEs).
“Tumebaini upungufu mkubwa wa alama za usalama na vifaa kinga. Afya ya mfanyakazi ndiyo mtaji wa mwekezaji, hivyo tutafanya ukaguzi wa kina na kutoa ushauri wa lazima ili mazingira haya yawe salama,” alisisitiza Bi. Mwenda.
Serikali imewahakikishia wawekezaji kuwa itaendelea kuwalinda na kuwapa ushirikiano, lakini haitafanya mzaha na haki za msingi za wafanyakazi. Maelekezo yametolewa kwa watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuhakikisha kila kiwanda mkoani Pwani kinakuwa kioo cha uzalishaji unaozingatia utu.
Ujumbe kwa wawekezaji ni mmoja: Boresha mazingira, mpe mfanyakazi mkataba na haki zake, naye atakupa faida na tija unayoitafuta.

No comments:
Post a Comment