Zaidi ya kilo 6,750,000 za pamba mbegu zinatarajiwa kuzalishwa katika wilaya za Mbogwe na Bukombe katika msimu wa kilimo wa mwaka 2025/2026, endapo wakulima watachukua na kupanda mbegu zote zilizotolewa, hatua inayotarajiwa kuongeza kipato cha wakulima na kukuza uchumi wa vyama vya ushirika.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 8 wa Chama Kikuu cha Ushirika Mbogwe na Bukombe uliofanyika leo Februari 6, 2026, Mwenyekiti wa chama hicho Said Tangawizi amesema uzalishaji huo unatarajiwa kupatikana kutoka katika ekari 45,000 zitakazolimwa na wakulima kutoka halmashauri za Mbogwe na Bukombe.
Ameeleza kuwa matarajio hayo ni sehemu ya mkakati wa chama wa kuimarisha zao la pamba na kuhakikisha wakulima wananufaika moja kwa moja na juhudi zao za uzalishaji.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti huyo amesema katika mwaka wa fedha 2026/2027, chama kinatarajia kununua na kuchambua pamba katika kiwanda cha MBCU LTD kilichopo Masumbwe wilayani Mbogwe, kwa lengo la kuongeza mapato ya chama na wakulima wa pamba. Kwa mujibu wa mpango huo, chama kinatarajia kununua pamba jumla ya kilo 5,000,000 zenye thamani ya shilingi 9,552,979,000 kutoka kwa wakulima wa Mbogwe, Bukombe pamoja na maeneo mengine.
Akitaja mafanikio yaliyopatikana katika msimu uliopita, amesema chama kimefanikiwa kutoa ajira kwa vijana na akina mama katika kipindi chote cha uzalishaji wa pamba, pamoja na kuhakikisha malipo kwa wakulima yanafanyika kwa wakati, jambo lililosaidia kuongeza imani ya wakulima kwa chama.
Hata hivyo, amesema chama kinakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo kuchelewa kupatikana kwa mikopo ya kununulia pamba kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), kuyumba kwa soko la pamba nyuzi na pamba mbegu, pamoja na kupanda kwa gharama za uendeshaji wa zao na uchambuaji wa pamba kunakosababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta ya petroli.
Mkutano Mkuu wa 8 umejadili namna ya kukabiliana na changamoto hizo kwa kushirikiana na serikali na wadau wa sekta ya kilimo ili kuendeleza zao la pamba kwa tija na manufaa ya wakulima.











No comments:
Post a Comment