TFF KUJENGA KITUO CHA KUKUZA VIPAJI KAHAMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 25 February 2026

TFF KUJENGA KITUO CHA KUKUZA VIPAJI KAHAMA


Na Neema Nkumbi, Kahama


Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, amesema shirikisho hilo linatarajia kujenga kituo cha kukuza vipaji vya mpira wa miguu katika Wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, katika eneo lililokuwa mgodi wa Buzwagi.

Karia ameyasema hayo leo februari 25,2026 alipokuwa akizungumza na wadau wa michezo wilayani Kahama, ambapo ameeleza kuwa miundombinu iliyopo pamoja na ukubwa wa eneo hilo vinafaa kwa ujenzi wa kituo kikubwa cha kukuza vipaji nchini, huku TFF ikiahidi kuanza maandalizi ya taarifa muhimu zitakazowezesha utekelezaji wa mradi huo.

Amesema sambamba na kukuza vipaji vya mpira wa miguu, watoto watakaopata nafasi ya kujiunga na kituo hicho wataendelea na masomo yao ya kawaida ili kuhakikisha wanapata elimu rasmi pamoja na mafunzo ya michezo.

Aidha, Karia amesema TFF inapanga kuendesha kozi za ukocha wilayani Kahama ili kuwajengea uwezo makocha wa ndani na kusaidia kukuza kiwango cha mpira wa miguu katika eneo hilo na nchini kwa ujumla.

Kwa mujibu wa taarifa ya awali ya wataalamu kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kahama iliyosomwa Afisa michezo wa Manispaa ya kahama Mwaita Mwinyimkuu, amesema walipotembelea eneo la Buzwagi Februari 18, 2026, eneo hilo lina miundombinu mbalimbali inayoweza kutumika kwa ajili ya kituo cha kukuza vipaji cha TFF (Sports Academy Centre).

Miundombinu hiyo inajumuisha viwanja vya michezo ikiwemo uwanja mkubwa wa mpira wa miguu wenye ukubwa wa mita za mraba 8,712 (urefu mita 132 na upana mita 66), maeneo ya kupumzikia, kiwanja cha netiboli, kiwanja cha mpira wa kikapu pamoja na kiwanja cha mpira wa wavu.

Aidha, eneo hilo lina ukumbi wa mazoezi ya ndani (Gym) wenye vifaa vya kisasa na vilivyo katika hali nzuri, utakaosaidia mazoezi ya wanamichezo watakaokuwa wakitumia kituo hicho.

Katika upande wa malazi, kuna nyumba 40 zinazoweza kuchukua watu kati ya 160 hadi 200 kwa kuzingatia matumizi ya vyumba viwili hadi vinne kwa kila nyumba, pamoja na mabweni ya vijana (Junior Hostels) yenye majengo 16 yenye vyumba 18 kila moja, yanayoweza kuhudumia hadi watoto au wanamichezo 288 kwa wakati mmoja.

Vilevile, kuna ofisi mbalimbali zinazoweza kutumika kwa shughuli za kiutawala za kituo, madarasa yatakayosaidia kuwapatia watoto elimu pamoja na kumbi ndogo za mikutano kwa matumizi ya viongozi na wadau wa michezo.

Miundombinu ya vyoo na mabafu nayo ipo katika hali nzuri na inatarajiwa kutumika na wataalamu pamoja na wanamichezo watakaokuwa kituoni hapo.

Wataalamu wamependekeza kufanyika kwa maboresho madogo ya baadhi ya miundombinu ili kuongeza ufanisi na kuwezesha eneo hilo kutumika rasmi kama kituo cha michezo kwa vijana na watoto.

Ujenzi wa kituo hicho unatarajiwa kuwa fursa muhimu kwa vijana wa Kahama na maeneo jirani kukuza vipaji vyao na kuimarisha maendeleo ya mpira wa miguu nchini.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso