TANESCO YATAKIWA KUHARAKISHA USIMIKAJI NGUZO, KUIMARISHA USHIRIKIANO NA VIONGOZI KAHAMA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Tuesday, 17 February 2026

TANESCO YATAKIWA KUHARAKISHA USIMIKAJI NGUZO, KUIMARISHA USHIRIKIANO NA VIONGOZI KAHAMA



Na Neema Nkumbi, Kahama



Mbunge wa Kahama Mjini, Benjamin Ngayiwa, ameutaka uongozi wa TANESCO kuhakikisha nguzo za umeme zinazowekwa katika maeneo mbalimbali zinasimikwa kwa wakati ili kuepusha malalamiko ya wananchi na kuimarisha imani kwa jamii.


Ngayiwa amesema hayo leo februari 17, 2025 katika kikao cha tanesco na wadau ambapo ameeleza kuwa kumekuwa na changamoto ya nguzo kukaa kwa muda mrefu bila kusimikwa hali inayosababisha maswali kwa wananchi, hivyo amesisitiza umuhimu wa utekelezaji wa haraka wa miradi hiyo.


Aidha, ameitaka TANESCO kuhakikisha inapohamisha nguzo au kutekeleza miradi, wanawasiliana na madiwani wa maeneo husika ili viongozi hao wawe na taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu mipango na utekelezaji wa miradi.


Mbunge huyo pia amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa umeme hadi katika vitongoji vingi vya Kahama, ambapo Katika Jimbo la Kahama, Jumla ya vitongoji ni 135, Hadi Kufikia Mwezi Juni, 2026 vitongoji vyenye Umeme vitakuwa 87 na visivyo na umeme 48.



“Endeleeni kuhakikisha vitongoji vilivyobaki vinapata umeme ili wananchi waweze kuongeza shughuli za kiuchumi,” amesema Ngayiwa.


Sambamba na hilo, amewasihi wananchi kulinda miundombinu ya umeme ikiwemo nguzo na nyaya ili kuepuka ajali za umeme na kukatika kwa huduma. Amewataka viongozi kushirikiana kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kulinda miundombinu hiyo.


Kwa upande wake, Meya wa Manispaa ya Kahama, Kaniki, amegusia changamoto ya ukatikaji wa umeme akisema amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi, lakini akawapongeza wahandisi wa TANESCO Kahama kwa kuwa wasikivu wanapopewa taarifa za hitilafu.


Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Absalum, ameishukuru TANESCO kwa kutoa elimu kwa madiwani akiwaita kuwa ni “majembe wa manispaa” wanaosaidia kusimamia maendeleo katika kata zao.


Amepongeza pia Meneja wa TANESCO Wilaya kwa utendaji wake mzuri na kuomba aendelee kushirikiana na viongozi wa wilaya katika kuimarisha huduma ya umeme.


Absalum amemshukuru Rais Samia kwa kuwezesha vitongoji 295 katika wilaya hiyo kupata umeme, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi ya nishati safi na kulinda miundombinu ya umeme.


Aidha, ameitaka TANESCO kuhakikisha wanatoa taarifa mapema kupitia vyombo vya habari pale panapotokea au panapotarajiwa kukatika kwa umeme, pamoja na kushirikisha madiwani kabla ya wakandarasi kuanza miradi katika maeneo yao.


Pia ameeleza kuwa bado kuna shule na zahanati kadhaa hazijapatiwa umeme, hivyo ameomba taasisi hizo kupewa kipaumbele.


Katika hatua nyingine, ameonya juu ya uwepo wa matapeli wanaojitambulisha kama watumishi wa TANESCO na kuwaibia wananchi, akitaka shirika hilo kushirikiana na viongozi wa kata kutoa elimu na tahadhari kwa wananchi ili kuepuka matukio hayo.





Mwisho.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso