TAFORI YAFUNGUA MILANGO YA AJIRA KWA VIJANA KUPITIA MITI YA ASILI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 13 February 2026

TAFORI YAFUNGUA MILANGO YA AJIRA KWA VIJANA KUPITIA MITI YA ASILI





Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) imekuja na mkakati mpya wa kufanya utafiti wa miti ya asili yenye thamani kubwa, hatua inayotajwa kuwa ni mkombozi wa ajira kwa vijana nchini.


Mkurugenzi Mkuu wa TAFORI, Dk. Revocatus Mushumbusi, amebainisha kuwa taasisi hiyo inajielekeza katika kuzalisha mbegu na miche ya asili kama mkongo, mninga na mpingo kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya maabara (vikonyo).



Lengo la mkakati huo ni kuhakikisha miti hiyo ambayo ipo hatarini kutoweka inapatikana kwa wingi, jambo linalofungua fursa kwa vijana kuanzisha vitalu vya biashara na mashamba ya miti ya asili ambayo mbao zake zina thamani kubwa sokoni.

Dk. Mushumbusi ameeleza kuwa utafiti unaonyesha miti ya asili inauwezo wa kukua haraka kama miti ya kigeni iwapo itapandwa mashambani na kupata matunzo stahiki.

Kwa maneno mengine hii ni fursa adhimu kwa vijana kujiajiri kama washauri wa kitaalamu wa misitu au wazalishaji wa miche, badala ya kusubiri ajira za ofisini. Aidha, mti kama mkongo una manufaa mengi kuanzia utengenezaji wa samani bora, vifaa vya muziki, hadi matumizi ya dawa za asili, hali inayotengeneza mnyororo mpana wa thamani ambao vijana wanaweza kuutumia kujipatia kipato endelevu.

Katika kuunga mkono juhudi hizo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, amewahimiza vijana kutumia fursa zinazotolewa na taasisi za serikali kama TAFORI ili kujiinua kiuchumi.

Msigwa amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imeweka mazingira wezeshi na kutoa kipaumbele kwa vijana, hivyo wanapaswa kutumia utaalamu na tafiti zinazofanywa na wataalamu wetu kama chanzo cha kujikomboa.

Kwa kuchangamkia kilimo cha miti ya asili, vijana watakuwa wanatekeleza kauli mbiu ya uzalendo ni kutunza mazingira, huku wakijitengenezea utajiri kupitia "Dhahabu ya Kijani" ya misitu ya Tanzania.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso