Na Neema Nkumbi, Dodoma
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu kama Mwana FA, ametangaza kupunguzwa kwa kiasi kikubwa ada za usajili kwa watoa maudhui mtandaoni, akisema hatua hiyo inalenga kuweka mazingira wezeshi, kuongeza ushindani na kuboresha upatikanaji wa taarifa sahihi kwa umma.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Vyombo vya Utangazaji (Annual Broadcasters’ Conference – ABC) 2026 uliofanyika leo, Mwinjuma amesema ada ya leseni ya utoaji maudhui mtandaoni imepunguzwa kutoka shilingi 500,000 hadi 50,000, huku ada ya watoa maudhui ikishuka kutoka shilingi milioni moja hadi laki moja kwa mwaka.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa sekta ya habari, akisisitiza kuwa lengo ni kuwezesha na siyo kudhibiti.
“Kwa gharama hizi nafuu, tunaamini watoa maudhui wengi wataingia kwenye mfumo rasmi na hivyo kuongeza ufanisi, ushindani na kuhakikisha jamii inapata taarifa sahihi,” amesema Mwinjuma.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo ameagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Bodi ya Ithibati kuhakikisha utoaji wa leseni za utangazaji unazingatia mikataba na maslahi ya wafanyakazi wa vyombo vya habari.
Amesema amepokea taarifa kuwa baadhi ya vyombo havijalipa wafanyakazi mishahara kwa zaidi ya miezi sita, na kuagiza mamlaka husika kufuatilia suala hilo na kuwasilisha mrejesho ndani ya wiki moja.
“Nina taarifa kwamba kuna vyombo havijalipa wafanyakazi wake kwa zaidi ya miezi sita. Hili siyo suala la siasa, nataka mrejesho ndani ya wiki moja,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Watangazaji Huru Tanzania (NIBA), Amos Ngosha, ameomba Serikali kupunguza wingi wa tozo zinazoikabili sekta hiyo, akieleza kuwa vyombo vya habari hulipa zaidi ya tozo 19 kila mwaka chini ya sheria tofauti, hali inayodhoofisha uwezo wao kifedha na kusababisha baadhi kushindwa kuendelea na huduma au kufungiwa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dkt. Jabir Bakari, amesema mwaka 2025 jumla ya wanahabari 2,054 wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo, huku usikivu wa redio ukifikia asilimia 85 na usambazaji wa televisheni kupitia satelaiti kufikia asilimia 100.
Aidha, hadi Desemba 2025, jumla ya leseni 770 za utangazaji zilikuwa zimetolewa, huku TCRA ikiwa na mpango wa kuanzisha mfumo wa redio kidijitali ili kuendana na maendeleo ya teknolojia na mahitaji ya soko la mawasiliano










































No comments:
Post a Comment