MKUU wa Mkoa wa Songwe, Jabiri Makame amewataka vijana mkoani humo na Tanzania kwa ujumla kutambua kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira rafiki na fursa nyingi ambazo hazijawahi kushuhudiwa katika awamu nyingine yoyote nchini.
Akizungumza katika Kongamano la 100 ya Tabasamu lililofanyika mkoani Songwe hivi karibuni, RC Makame alisema kuwa vijana wanapaswa kujivunia uongozi wa Rais Samia kutokana na jitihada zake za makusudi za kutengeneza mazingira bora ya kiuchumi na kijamii kwa kundi hilo.
Alibainisha kuwa, katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge la 13, Rais Samia aligusia kwa kina masuala yanayohusu vijana, akisisitiza jinsi ya kuendeleza vipaji na kufungua milango ya fursa mbalimbali kwa ajili ya maendeleo yao.
“Hakuna awamu ya uongozi wa nchi hii ambayo vijana wanapaswa kujivunia kama awamu ya sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan. Rais amefanya kila linalowezekana kutengeneza mazingira bora kwa vijana ili waweze kujikwamua kiuchumi na kukuza vipaji vyao,” alisema RC Makame.
AMANI NI MSINGI WA RIZIKI
Katika hatua nyingine, wananchi mkoani Pwani wametoa wito kwa Watanzania kudumisha amani na mshikamano, wakisema kuwa bila utulivu hakuna shughuli yoyote ya kimaendeleo inayoweza kufanyika.
Akizungumza mjini Kibaha, Kawiya Manyamba, ambaye ni fundi wa kushona katika eneo la Maili Moja, alisema amani ni tunu ambayo kila mwananchi anapaswa kuilinda kwa gharama yoyote ili kuendelea kupata riziki za kila siku.
“Nawaomba Watanzania tudumishe amani ambayo ni tunu tuliyopewa na Mwenyezi Mungu. Tuwe na uvumilivu ili tuendelee kupata riziki zetu, kwani kama hakuna amani hatuwezi kupata riziki na tuendeleze mshikamano wetu,” alisema Manyamba.
Naye mjasiriamali kutoka Kibaha Mjini, Said Ng’ombe, alisisitiza kuwa amani ndiyo kiungo kikuu cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwani kuvunjika kwa amani kunasababisha watu kukosa muda wa kufanya shughuli zao za kila siku.
Kwa upande wake, Jabir Makasala, mkazi wa Kibaha, alitoa wito kwa kila Mtanzania kuiombea nchi amani ili utulivu uendelee kutawala. Alisema kuwa utulivu unawafanya wananchi kuwa huru na kuongeza mshikamano wa kufanya maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Wito huo wa wananchi unakuja wakati ambapo Serikali inaendelea kusisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa kama nguzo kuu ya kufikia malengo ya kiuchumi yaliyowekwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa.

No comments:
Post a Comment