Na Neema Nkumbi, Kahama
Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Azan Mufti, amesema kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa shirikisho hilo katika Wilaya ya Kahama ni heshima kubwa kwa wakazi wa eneo hilo na mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.
Mufti ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya mkutano huo unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 na 28 Februari 2026, ukiwa ni mara ya kwanza kwa TFF kufanya mkutano wake wa kawaida katika wilaya hiyo.
Amesema mkutano huo utawakutanisha zaidi ya wajumbe 400 kutoka maeneo mbalimbali ya nchi, ambao watapata fursa ya kubadilishana mawazo, kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya soka na kuweka mikakati mipya ya kuendeleza mpira wa miguu nchini.
Mufti ameongeza kuwa miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni mpango wa ujenzi wa uwanja wa kisasa utakaokuwa na uwezo wa kuchukua zaidi ya mashabiki 7,000, hatua itakayochochea maendeleo ya soka katika Wilaya ya Kahama na maeneo ya jirani.
Aidha, amewataka wananchi wa Kahama kujitokeza kwa wingi kuupokea mkutano huo kwa moyo wa ushirikiano na kutumia fursa za kiuchumi zitakazotokana na ujio wa wageni wengi, wakiwemo viongozi wakuu wa soka nchini.
Pia amewahimiza vijana kushiriki katika shughuli mbalimbali zitakazoambatana na mkutano huo ili kujifunza na kunufaika na uzoefu wa viongozi na wadau wa soka watakaokuwepo.
Kwa mujibu wa Mufti, Rais wa TFF, Wallace Karia, anatarajiwa kuwasili Kahama Februari 25 kwa ajili ya kukamilisha maandalizi ya mwisho kabla ya mkutano huo kuanza rasmi.
Awali, mkutano huo ulikuwa umepangwa kufanyika Februari 21 mwaka huu, lakini ukaahirishwa na kupangwa upya kufanyika Februari 27 na 28, 2026.


No comments:
Post a Comment