KUTOKA KEJERI ZA MITANDAONI HADI UBUNIFU WA KIVIWANDA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 11 February 2026

KUTOKA KEJERI ZA MITANDAONI HADI UBUNIFU WA KIVIWANDA



KATIKA hali inayolenga kuleta mapinduzi ya kifikra miongoni mwa vijana nchini, Serikali imewataka wasomi na wabunifu kuacha kutumia nguvu na elimu yao kukejeli viongozi na mifumo ya nchi mitandaoni, badala yake wajikite katika kutatua changamoto za kijamii kupitia sayansi na teknolojia.

Hayo yamebainishwa wakati kukiwa na msisitizo mpya wa kuunganisha mfumo wa elimu na mahitaji halisi ya soko la ajira, ambapo Serikali imeweka wazi kuwa sifa ya kwenda shule inapaswa kuonekana kupitia uwezo wa mhitimu kutatua matatizo ya nchi na si malumbano yasiyo na tija.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, akizungumza jijini Dar es Salaam, amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya vyuo na sekta ya uzalishaji (viwanda) si suala la hiari tena, bali ni wajibu wa kimfumo. Alisema hatua hiyo inalenga kuhakikisha stadi zinazofundishwa zinawiana na soko la ajira ili kumfanya mhitimu awe tayari kuajiriwa au kujiajiri mara moja.

“Sera ya elimu inabainisha wazi; ushirikiano huu ni lazima ili kuchochea ukuaji wa uchumi. Wizara imesaini mikataba zaidi ya 370 kati ya taasisi za elimu (VETA, Vyuo vya Ufundi na Elimu ya Juu) na viwanda ili kuziba pengo la ujuzi wa vitendo,” alisema Mhe. Wanu.

Naye Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, aliongeza kuwa tafiti zinaonyesha bado kuna pengo kati ya nadharia za darasani na mahitaji ya viwandani. Alisema waajiri wanahitaji wahitimu wenye maadili ya kazi, ubunifu, na uwezo wa kutumia teknolojia za kisasa, na si tu vyeti vya kutaaluma.

Fursa katika Nishati Safi

Wakati elimu ikifanyiwa maboresho, sekta ya mazingira imetajwa kuwa shamba jipya la ajira kwa vijana wabunifu. Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amewahimiza vijana na sekta binafsi kuwekeza katika teknolojia ya magari yanayotumia umeme ili kupunguza matumizi ya mafuta na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Dkt. Muyungi alisema Serikali inathamini wabunifu wa nyenzo zinazopunguza gesijoto na inashirikiana na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kuweka mikakati ya kusaidia usafiri wa umeme nchini. Hii inatajwa kuwa ni fursa adhimu kwa vijana wenye stadi za ufundi na umeme (Electrical Engineering) kuanzisha vituo vya kuchajia na huduma za matengenezo.

Ujumbe kwa Vijana Wachambuzi wa masuala ya jamii wanasema hatua hizi za Serikali ni njia nyeupe kwa vijana wanaolalamikia ukosefu wa ajira. Badala ya kupoteza muda mitandaoni kuonyesha kuwa watu hawajaenda shule kwa kejeli, njia ya sasa ni kutumia elimu hiyo kuingia katika mikataba ya ushirikiano na viwanda, kubuni teknolojia rafiki wa mazingira, na kutumia majukwaa ya kidijiti kama 'Fursa Hub' kupata mitaji.

"Ubunifu ni kutatua changamoto ya gesijoto au kubuni mtaala wa vitendo, si matusi mtandaoni," alisema mmoja wa wadau wa maendeleo jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso