HALMASHAURI YA USHETU YAPITISHA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 45.3 KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO 2026/2027 - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Thursday, 5 February 2026

HALMASHAURI YA USHETU YAPITISHA BAJETI YA SHILINGI BILIONI 45.3 KWA UTEKELEZAJI WA MIRADI YA MAENDELEO 2026/2027



Halmashauri ya Ushetu Yapitisha Bajeti ya Shilingi Bilioni 45.3 kwa Utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo

Na Neema Nkumbi, Kahama



Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu imepitisha bajeti ya shilingi bilioni 45.3 kwa mwaka wa fedha 2026/2027, fedha zinazotarajiwa kutumika kutekeleza miradi yote ya maendeleo iliyopangwa, ikijumuisha mapato ya ndani pamoja na fedha kutoka Serikali Kuu.

Akizungumza leo Februari 5, 2026 katika kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika wilayani humo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu, Bi. Hadija Kabojela, amesema bajeti hiyo imelenga kugusa moja kwa moja maisha ya wananchi kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta muhimu ikiwemo elimu, afya, miundombinu pamoja na miradi ya ngazi ya kata.

Bi. Kabojela amewasisitiza watumishi wote wa halmashauri kusimamia kwa uadilifu na weledi matumizi ya fedha hizo, akibainisha kuwa lengo ni kuhakikisha kila shilingi inaleta tija na kuboresha huduma kwa wananchi.

Amesema katika uandaaji wa bajeti hiyo, halmashauri imezingatia kauli ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliyotoa wakati wa uzinduzi wa Bunge la Kumi na Tatu, akisisitiza umuhimu wa “kupeleka tabasamu kwa wananchi.”

“Kupitia bajeti hii, tumelenga kukamilisha maboma mbalimbali yaliyoanzishwa na wananchi kwa nguvu zao wenyewe, ambapo mapato ya ndani ya halmashauri yatatumika kusaidia kukamilisha miradi hiyo,” amesema Bi. Kabojela.

Aidha, amesema bajeti hiyo imezingatia vipaumbele vyote vilivyopo katika Dira ya Maendeleo ya Taifa pamoja na mahitaji halisi ya wananchi wa Wilaya ya Ushetu, kwa lengo la kuimarisha maendeleo endelevu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Ushetu ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Igwamanoni, Gagi Lala Gagi, amesema bajeti ni mchakato unaohusisha hatua mbalimbali, akieleza kuwa ilianza kujadiliwa katika kamati za halmashauri kabla ya kufikishwa katika baraza kwa ajili ya uamuzi wa mwisho.

Amesema baada ya kupitia mapendekezo na kufanya maboresho katika ngazi ya kamati, Baraza la Madiwani limefanya hitimisho kwa kuipitisha rasmi bajeti hiyo kwa maslahi mapana ya wananchi wa wilaya hiyo.

Naye Diwani wa Kata ya Bukomela, Kulwa Shoto, amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ushetu kwa kuwa na mahusiano mazuri na watendaji wake, jambo ambalo limechangia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa bajeti yenye ubora na mwelekeo mzuri wa maendeleo.

Amesema ushirikiano mzuri kati ya uongozi wa halmashauri na watendaji umeiwezesha halmashauri kuandaa bajeti inayogusa mahitaji halisi ya wananchi, hali iliyowasukuma madiwani kuipitisha bajeti hiyo kwa kauli moja.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso