HALMASHAURI YA MANISPAA YA KAHAMA YAVUNJA MKATABA WA MKANDARASI WA BARABARA ZA TACTIC - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Friday, 6 February 2026

HALMASHAURI YA MANISPAA YA KAHAMA YAVUNJA MKATABA WA MKANDARASI WA BARABARA ZA TACTIC



Halmashauri ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga imevunja rasmi mkataba wake na Mkandarasi Kampuni ya Sichuan Road and Bridge Construction Limited aliyekuwa akitekeleza mradi wa ujenzi wa barabara za mjini Kahama zenye urefu wa kilomita 15.2 kupitia Mpango wa Uboreshaji wa Miji Tanzania (TACTIC), baada ya kutoridhishwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa mradi huo.

Akizungumza wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa hiyo, Masud Kibetu, amesema uamuzi wa kuvunja mkataba umefikiwa baada ya mkandarasi huyo kuongezewa muda wa ziada kwa zaidi ya mara tatu bila mafanikio ya kuridhisha katika utekelezaji wa mradi.

Kibetu amesema mkataba wa ujenzi wa barabara hizo ulisainiwa mwezi Novemba 2023, ambapo mkataba wa awali ulipaswa kukamilika tarehe 19 Februari 2025. Hata hivyo, kutokana na mkandarasi kushindwa kukamilisha kazi kwa wakati, Halmashauri ililazimika kuongeza muda mara kadhaa, huku mwisho wa mkataba wa kawaida na wa adhabu ukiwa tarehe 15 Januari 2026.

Ameeleza kuwa hadi kufikia tarehe 15 Februari 2025, mkandarasi alikuwa amekamilisha ujenzi wa kilomita 1.7 pekee kati ya kilomita 15.2 zilizokuwa kwenye mkataba, hali iliyochangia Halmashauri kuchukua hatua za kisheria baada ya taratibu zote kukamilika.

“Baada ya kupitia taratibu zote, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama imevunja rasmi mkataba na mkandarasi huyo tarehe 19 Januari 2026,” amesema Kibetu.

Aidha, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema kuwa hatua za kumpata mkandarasi mwingine zitakazokamilisha ujenzi wa barabara hizo zinaendelea, ili kuhakikisha wananchi wa Manispaa ya Kahama wanapata miundombinu bora kama ilivyokusudiwa.

Awali, Diwani wa Viti Maalumu wa Manispaa ya Kahama, Herieth Makaga, amehoji juu ya hatua zinazochukuliwa na Halmashauri kuwanusuru wananchi wanaotaabika na ubovu wa barabara za mjini Kahama, licha ya kuwepo kwa mkandarasi aliyekuwa amepewa zabuni ya utekelezaji wa mradi huo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso