BILIONI 4.6 ZA SAMIA: USHINDI MWINGINE WA SERIKALI KATIKA KUTATUA CHANGAMOTO YA AJIRA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Monday, 16 February 2026

BILIONI 4.6 ZA SAMIA: USHINDI MWINGINE WA SERIKALI KATIKA KUTATUA CHANGAMOTO YA AJIRA

 



Katika mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na utulivu wa kiuchumi na usalama wa ajira kwa vijana, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na taasisi ya Benki ya CRDB (CRDB Bank Foundation), zimetenga Shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya kuwezesha miradi bunifu nchini kupitia ‘Mfuko wa Samia’.


Hatua hiyo inatajwa kuwa ni mwendelezo wa juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kutengeneza mazingira wezesha ya ajira, jambo ambalo ni nguzo kuu ya kudumisha amani na utulivu. Fedha hizo ni mchango sawa wa Shilingi bilioni 2.3 kutoka kila upande, zikilenga kugeuza mawazo ya kiteknolojia kuwa biashara halisi zinazozalisha ajira.


Akizindua programu hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir, alisema serikali inatambua kuwa kuwapa wananchi mikopo inayoambatana na maarifa ni chachu ya mabadiliko chanya. Alisisitiza kuwa uwezeshaji huo ni dhamira ya dhati ya kuthaminisha ubunifu wa ndani ili kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi.


“Nawaomba COSTECH na CRDB Bank Foundation mhakikishe mnawafikia wabunifu wengi kadri iwezekanavyo. Kwa kutumia ubunifu wa ndani, Tanzania inaweza kutatua changamoto zake bila kuhitaji maarifa kutoka nje,” alisema Wanu, akibainisha kuwa uthubutu huu unalenga kuinua hali ya maisha ya Watanzania kote nchini.


Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Benki ya CRDB, Tully Mwambapa, alieleza kuwa ushirikiano huo ni ushahidi wa nguvu ya sekta binafsi inapoungana na serikali kuwahudumia wananchi. Alibainisha kuwa mfuko huo ni suluhu ya muda mrefu ya kuondoa changamoto ya ukosefu wa mitaji iliyokuwa ikisababisha mawazo mengi ya vijana kufifia na hivyo kuhatarisha usalama wao wa ajira.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dk. Amos Nungu, aliongeza kuwa Mfuko wa Samia umekuja kusaidia biashara changa kupiga hatua kutoka maabara kuelekea sokoni. Alisema uamuzi huo ulifikiwa baada ya kuona uwepo wa kizazi cha vijana wenye uwezo mkubwa wa kubadili mwelekeo wa uchumi wa taifa ikiwa wataungwa mkono na mifumo rafiki na mitaji yenye masharti nafuu.


Hata hivyo, wadau wa kijamii na kiuchumi wamehusisha uwezeshaji huo na hitaji la kudumisha amani ya nchi. Mwenyekiti wa SHIVYAWATA Kibaha Mjini, Jabir Makasala, alitoa wito kwa Watanzania kuiombea nchi amani akisisitiza kuwa bila utulivu hakuna maendeleo yanayoweza kufanyika, huku akibainisha kuwa amani ndiyo inayomfanya kila mmoja kuwa huru kutafuta ridhiki yake.


Sauti hizo ziliungwa mkono na Alex Msimbe, Naibu Katibu Mkuu wa Soko la Loliondo Kibaha, aliyesema kuwa amani ni mtaji namba moja kwa wafanyabiashara. Aliongeza kuwa mshikamano wa kitaifa ndio utakaowezesha miradi kama hii ya uwezeshaji vijana kufanikiwa na kuleta tija iliyokusudiwa katika kukuza kipato cha mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.


Hadi kufikia Julai 2025, jumla ya maombi 152 yalikuwa yamepokelewa katika dirisha la mpito la mfuko huo, ikiwa ni ishara ya kiu kubwa ya vijana katika kujiajiri na kuchangia katika uchumi wa kisasa, huku wakitakiwa kuepuka ushawishi wa vurugu na badala yake kulinda utulivu uliopo kwa ajili ya ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso