TIMU ya Bandari Tanzania imeanza vema msimu wa Ligi daraja la pili baada ya kumaliza mzunguko wa kwanza kwa kukusanya jumla ya pointi 17 katika Kundi A, hatua inayowaweka katika nafasi nzuri ya kuwania mafanikio zaidi msimu huu.
Baada ya kuifunga Dar City kwa mabao 4-0, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Omega Seme, kwa kushirikiana na benchi la ufundi, amewaruhusu wachezaji kwenda mapumziko ya siku nane ili kuwapa nafasi ya kupumzika na kurejesha nguvu kabla ya kuendelea na ratiba ya ligi.
Akizungumza baada ya kukamilika kwa mzunguko wa kwanza, uongozi wa timu hiyo umeeleza kuridhishwa na mwenendo wa kikosi, huku ukimpongeza Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Ismail Chimpele, kwa kuhakikisha mazingira mazuri kwa wachezaji na benchi la ufundi, hali iliyosaidia timu kufanya vizuri kulingana na mipango iliyowekwa.
Imeelezwa kuwa baada ya mapumziko hayo, Bandari Tanzania itarejea kambini jijini Dar es Salaam Februari 9, mwaka huu, kuanza maandalizi ya mechi za mzunguko wa pili wa ligi pamoja na michuano ya Kombe la Shirikisho la CRDB. Msimu huu pia ni wa kipekee kwa klabu hiyo kutokana na ushiriki wao katika mashindano ya Pan African, huku Machi 14 ikitarajiwa kuwa siku muhimu baada ya kurejea nyumbani.
Kuhusu usajili wa dirisha dogo, uongozi wa klabu umeeleza kuwa bado haujaamua kufanya mabadiliko makubwa, bali utaangalia maeneo machache ya kuimarisha kikosi ili kufanya vizuri zaidi kwenye mzunguko wa pili ukilinganisha na mwanzo wa msimu.
Bandari Tanzania imetoa shukrani za dhati kwa mashabiki wake kote nchini kwa kuendelea kuipa sapoti kubwa timu hiyo, ikisisitiza kuwa uongozi unaendelea kufanya kazi kuhakikisha klabu inazidi kuimarika na kuleta matokeo chanya.
Habari hii imetolewa na Ofisa Habari wa Bandari Tanzania, Philipo Chimi.

No comments:
Post a Comment