Na Neema Nkumbi, Kahama.
Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Glory Absalum, ametoa wito kwa wanachama wa chama cha ushirika wilayani humo kuzingatia uadilifu, uaminifu na sheria za ushirika ili kuondoa migogoro inayoendelea kujitokeza, hususan wakati wa msimu wa mauzo ya tumbaku.
Akizungumza leo Januari 30, 2026, katika Mkutano Mkuu wa 30 wa Mwaka wa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU LTD), Absalum amesema migogoro mingi inayojitokeza inasababishwa na kutokuzingatia maadili, ikiwemo kuchanganya tumbaku bila kufuata madaraja husika, hali inayosababisha kushuka kwa bei na kuibua sintofahamu kati ya chama cha ushirika na wanunuzi.
“Niwaombe wanaushirika kuwa waaminifu wakati wa kufunga tumbaku kulingana na madaraja yake, kwani kuchanganya tumbaku kunasababisha migogoro na hatimaye kushusha bei sokoni,” amesema Absalum.
Aidha, amewataka wakulima kuuza mazao yao kupitia vyama walivyojisajili badala ya kuyauza kwenye vyama vingine, akisema tabia hiyo inachochea migogoro na kudhoofisha mfumo wa ushirika, Pia ameonya wakulima dhidi ya utoroshaji wa tumbaku, akieleza kuwa husababisha kushindwa kurejeshwa kwa mikopo inayotolewa kupitia vyama vya ushirika.
“Chama cha ushirika kimeanzishwa kwa lengo la kuwasaidia wakulima, Mkianza kufanya ujanja ujanja, hamtafika mbali hivyo ni muhimu kuzingatia sheria na kanuni zinazotuongoza,” amesisitiza.
Katibu Tawala huyo pia amewahimiza wakulima kuzingatia kanuni bora za kilimo kwa kushirikiana na maafisa ugani waliopo katika maeneo yao, pamoja na kurasimisha na kuendeleza kilimo cha mazao mengine ili kupanua wigo wa uzalishaji na vyanzo vya kipato.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Kahama (KACU), Emanuel Nyambi, amesema chama hicho kimetambua changamoto zinazokikabili na tayari kimeanza kuchukua hatua za kuzitatua.
“Tunakuhakikishia kuwa maelekezo yote uliyoyatoa tunayafanyia kazi, Hata sisi tulishakaa pamoja, tukazichambua changamoto zetu, tukafanya tathmini na tumeweka mikakati madhubuti ya kuzitatua,” amesema Nyambi.
Mkutano huo uliwakutanisha viongozi wa vyama vya msingi, wakulima na wadau mbalimbali wa ushirika, ukiwa na lengo la kutathmini mwenendo wa chama na kuweka mikakati ya kuimarisha ushirika na ustawi wa wakulima wilayani Kahama.








No comments:
Post a Comment