MILANGO YA MAENDELEO YAFUNGUKA BAADA YA UJENZI WA DARAJA LA UBAGWE II, WANANCHI USHETU WAELEZA ADHA WALIZOKUWA WANAPITIA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 25 January 2026

MILANGO YA MAENDELEO YAFUNGUKA BAADA YA UJENZI WA DARAJA LA UBAGWE II, WANANCHI USHETU WAELEZA ADHA WALIZOKUWA WANAPITIA

  


Mwonekano wa madaraja yaliyojengwa na wakandarasi wazawa katika Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama

Na Neema Nkumbi - Kahama, Shinyanga

Wananchi wa Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama wameeleza kufaidika kwa kiwango kikubwa baada ya kukamilika kwa ujenzi wa Daraja la Ubagwe II, ambalo limeondoa changamoto ya usafiri na mawasiliano iliyokuwa ikiwakabili kwa miaka mingi hasa nyakati za mvua.

Kwa miaka mingi wananchi wa maeneo yanayozunguka mto Ubagwe walilazimika kutumia mitumbwi kuvuka mto huo, hali iliyohatarisha maisha yao na kusababisha ucheleweshaji wa huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Mkazi wa Ushetu, Idd Nkole, amesema kabla ya kujengwa kwa daraja hilo wananchi walikuwa wakikabiliwa na hatari kubwa wakati wa kuvuka mto, hasa kipindi cha mvua ambapo maji yalifurika na kufanya usafiri kuwa mgumu.

"Tulikuwa tunavushwa kwa mitumbwi na wakati mwingine tulilazimika kusubiri maji yapungue ndipo tuvuke. Ilikuwa ni hali ya hatari sana, lakini sasa tunapita bila shida yoyote, Serikali imetufanyia jambo kubwa sana," amesema Nkole.

Naye Zakaria Bundala amesema daraja hilo limekuwa mkombozi kwa wananchi wengi kutokana na kurahisisha usafiri wa wagonjwa, wanafunzi na wafanyabiashara.

"Maji yalipofurika kulikuwa hakuna namna ya kuvuka, Wajawazito walipata shida kufika hospitalini na watoto walikosa masomo, Sasa hali hiyo imekwisha, tunamshukuru Rais Samia kwa kutuletea maendeleo haya," amesema Bundala.

Wananchi wameeleza kuwa pamoja na kuimarika kwa usafiri, daraja hilo limechochea shughuli za biashara kwa kurahisisha usafirishaji wa mazao kutoka vijijini kwenda masokoni na kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa mradi huo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya madaraja ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Amesema Daraja la Ubagwe II ni miongoni mwa madaraja matatu yaliyojengwa katika Halmashauri ya Ushetu kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, ambapo miradi hiyo imegharimu zaidi ya shilingi bilioni 13.5 na imefikia asilimia 99 ya utekelezaji.

Kwa mujibu wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya, daraja hilo limejengwa kwa viwango vya kisasa ili kuhimili maji mengi ya mafuriko yaliyokuwa yakisababisha usumbufu mkubwa kwa wananchi.

Ujenzi wa Daraja la Ubagwe II unatajwa kuwa hatua muhimu ya serikali katika kuboresha miundombinu ya usafiri na kuunganisha wananchi wa Ushetu na maeneo mengine ya wilaya ya Kahama, jambo ambalo linatarajiwa kuongeza kasi ya shughuli za kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso