KIWANDA CHA MUSUMBA STEEL CHATAMBUA FURSA, SERIKALI YAAHIDI KUKIENDELEZA NA KUKILINDA DHIDI YA USHINDANI WA BIDHAA ZA NJE - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 10 January 2026

KIWANDA CHA MUSUMBA STEEL CHATAMBUA FURSA, SERIKALI YAAHIDI KUKIENDELEZA NA KUKILINDA DHIDI YA USHINDANI WA BIDHAA ZA NJE


KIWANDA CHA MUSUMBA STEEL CHATAMBUA FURSA, SERIKALI YAAHIDI KUKIENDELEZA NA KUKILINDA DHIDI YA USHINDANI WA BIDHAA ZA NJE

Baadhi ya bidhaa zinazozalishwa katika kiwanda cha Msumba Steel Tanzania Limited


Na Neema Nkumbi, Kahama


Serikali imeendelea kuonesha dhamira ya dhati ya kulinda na kukuza uwekezaji wa viwanda vya ndani, baada ya kuahidi kushughulikia changamoto zinazokikabili Kiwanda cha Musumba Steel Tanzania Limited kilichopo wilayani Kahama mkoani Shinyanga, hususan ushindani wa bidhaa za chuma zinazoingizwa kutoka nje ya nchi kwa bei ya chini.

Ahadi hiyo imetolewa Januari 10, 2026 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Stephen Chaya, wakati wa ziara yake ya kikazi katika Kongani ya Buzwagi, ambapo alitembelea pia kiwanda cha Musumba Steel kinachozalisha bidhaa mbalimbali za ujenzi ikiwemo mabati, misumari, mabomba pamoja na bidhaa nyingine za chuma.

Akizungumza baada ya kukagua uzalishaji katika kiwanda hicho, Dkt. Chaya amesema Musumba Steel ni mfano wa uwekezaji wenye tija unaoendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayotoa kipaumbele kwa uwekezaji wa ndani na nje ya nchi kama msingi wa kukuza viwanda, kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Taifa.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejipanga kuhakikisha wawekezaji waliopo wanalindwa, wanahudumiwa na wanakua kupitia taasisi zake ikiwemo Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Kiuchumi na Maeneo ya Viwanda Tanzania (TISEZA), ili waweze kufanya shughuli zao katika mazingira rafiki na yenye uhakika wa kisheria.

“Serikali imefungua milango kwa wawekezaji kutoka mataifa mbalimbali. Uwekezaji wa Musumba Steel unaomilikiwa na mwekezaji kutoka Burundi ni ushahidi kuwa Tanzania ni mahali salama pa kuwekeza. Changamoto zao tumezipokea na tutaendelea kushirikiana na wizara na taasisi husika kuzitatua,” amesema Dkt. Chaya.

Ameongeza kuwa wilaya ya Kahama ina fursa kubwa za uwekezaji kutokana na uwepo wa maeneo yaliyotengwa rasmi kwa ajili ya viwanda ikiwemo Kongani ya Buzwagi, sambamba na miundombinu muhimu kama umeme, maji, barabara na uwanja wa ndege, hali inayorahisisha uzalishaji na usafirishaji wa bidhaa.

Kwa upande wake, Meneja wa TISEZA Kanda ya Ziwa, Phina Jerome, amesema Musumba Steel Tanzania Limited ni miongoni mwa wawekezaji wakubwa wanaopata huduma za karibu kutoka TISEZA, akiwahimiza wawekezaji wengine kujisajili na kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo wilayani Kahama.

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Uwekezaji Binafsi kutoka Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Fadhili Chilumba, amesema masuala ya uwekezaji yanaongozwa na Sheria ya Uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Uchumi ya mwaka 2025, akisisitiza umuhimu wa kufuata sheria na sera sahihi ili kulinda wawekezaji na kuongeza ushindani wa viwanda vya ndani.

Akizungumza kwa niaba ya Musumba Steel Tanzania Limited, Mdhibiti Ubora na Meneja wa Mradi wa kiwanda hicho, Andrew Samwel, amesema kiwanda kilianzishwa mwaka 2024 na hadi sasa kimeajiri wafanyakazi 65, wengi wao wakiwa ni vijana wa Kitanzania, huku uwekezaji uliofanyika hadi sasa ukifikia zaidi ya shilingi bilioni 27.


Ameongeza kuwa kampuni ina mpango wa kuongeza uwekezaji huo hadi kufikia shilingi bilioni 35 ifikapo mwaka 2027, ikiwa ni pamoja na kuongeza mitambo, uzalishaji na aina za bidhaa za chuma zitakazokidhi mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, Samwel ametaja changamoto ya ushindani wa bidhaa za chuma zinazoingizwa kutoka nje kwa bei ya chini kuwa kikwazo kikubwa kwa ukuaji wa viwanda vya ndani, hali inayosababisha bidhaa zinazozalishwa nchini kukosa soko la uhakika.

“Tunaomba taasisi za Serikali kuunga mkono viwanda vya ndani kwa kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini. Hii italinda ajira za Watanzania, kukuza teknolojia ya ndani na kuongeza mapato ya Serikali,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, amesema uwepo wa kiwanda cha Musumba Steel ni chachu ya maendeleo ya wilaya hiyo, kwani kinatoa ajira, kinawaongezea vijana ujuzi wa kiteknolojia na kuchangia mapato ya Serikali, akiahidi kuendelea kuweka miundombinu wezeshi ili kuvutia uwekezaji zaidi.

Ziara hiyo imeacha matumaini mapya kwa wawekezaji wa ndani na nje, huku Musumba Steel ikitajwa kuwa nguzo muhimu ya safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu.



No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso