NA NEEMA NKUMBI, KAHAMA
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde, amesema Kongani ya Viwanda ya Buzwagi ni chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa Manispaa ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga na Taifa kwa ujumla, akibainisha kuwa utekelezaji wake utafungua fursa kubwa za ajira, uwekezaji na kukuza uchumi wa ndani.
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi katika eneo la kongani hiyo, Mhe. Mavunde amesema kuwa wakati wa uwepo wa Mgodi wa Buzwagi, Kahama ilinufaika kwa kiasi kikubwa kupitia mapato na ajira, hali inayotarajiwa kuongezeka maradufu kufuatia kuanzishwa kwa Kongani ya Viwanda ya Buzwagi.
Waziri Mavunde amesisitiza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia ametoa maelekezo ya kuhakikisha kongani hiyo inaanza kufanya kazi kwa haraka ili kuchangia jitihada za kurejesha na kukuza uchumi wa Taifa.
Waziri Mavunde amesema Serikali haitavumilia watu au makampuni yatakayochukua maeneo kwa lengo la kuyashikilia bila kuwekeza, akisisitiza kuwa kipaumbele kitapewa kwa wawekezaji watakaotekeleza miradi halisi. Ameeleza kuwa Serikali imelenga kuifanya Kahama kuwa kitovu cha utoaji wa huduma na bidhaa za migodini Kusini mwa Jangwa la Sahara, hatua itakayoongeza thamani ya rasilimali za madini na kuhakikisha mapato yanayopatikana yanabaki ndani ya nchi.
Ameongeza kuwa Serikali tayari imefanya marekebisho ya sheria na sera katika sekta ya madini na uwekezaji ili kuhakikisha Watanzania wananufaika moja kwa moja na rasilimali walizopewa na Mwenyezi Mungu. Kwa mujibu wa Waziri huyo, fedha zinazotarajiwa kubaki nchini kupitia uwekezaji huo zinakadiriwa kufikia takribani shilingi trilioni 5, hivyo kuna umuhimu wa kuweka mazingira rafiki yatakayovutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Waziri Mavunde ameongeza kuwa, ukiondoa Jiji la Dar es Salaam, Kahama ni miongoni mwa maeneo yanayokua kwa kasi kubwa katika uwekezaji nchini. Amefafanua kuwa wakati wa uendeshaji wa Mgodi wa Buzwagi kulikuwa na wafanyakazi wapatao 5,000 waliokuwa wakijihusisha zaidi na shughuli za uchimbaji, ilhali kongani hiyo inatarajiwa kuwa na zaidi ya viwanda 30 vitakavyoanzishwa, hali itakayoongeza kwa kiasi kikubwa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Katika hatua nyingine, Waziri Mavunde amesema Serikali ina mpango wa kujenga viwanda vitatu vya kutengeneza vilipuzi, ambavyo ni bidhaa muhimu zinazotumika kwa wingi katika shughuli za migodini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TSEZA), Gilead Teri, amesema kuwa mwekezaji yeyote atakayewasilisha maombi ya eneo la uwekezaji katika Kongani ya Buzwagi atapatiwa leseni ndani ya saa 24, akisisitiza kuwa lengo ni kuifanya Buzwagi kuwa kitovu cha biashara kutokana na ukaribu wake na nchi za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Rwanda, Burundi na Uganda.
Ameeleza kuwa eneo la Buzwagi Zone lina ukubwa wa hekta 1,333 na lina uwezo wa kuhimili uanzishwaji wa viwanda zaidi ya 30, hivyo ni muhimu kwa Wizara ya Madini kuendelea kuitangaza fursa hiyo ili malengo yaliyokusudiwa yafikiwe, huku akisisitiza kuwa Kahama inaweza kuwa kitovu
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita amesema kuwa wamejipanga vilivyo kuhakikisha kwamba kongani hii inaenda kufanikiwa na inakuwa ya mfano na kwamba wako mstari wa mbele kuweka mazingira wezeshi na miondo mbinu kuimarishwa huku tukihamasisha wananchi kwa kuwapa taarifa ya mema yanayoendelea katika kongani hiyo.












No comments:
Post a Comment