SHEKH WA WILAYA YA KAHAMA AWAHUSIA VIJANA KUDUMISHA AMANI, APONGEZA MICHEZO NA APENDEKEZA UPANUZI WA TAMASHA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 21 December 2025

SHEKH WA WILAYA YA KAHAMA AWAHUSIA VIJANA KUDUMISHA AMANI, APONGEZA MICHEZO NA APENDEKEZA UPANUZI WA TAMASHA








Shekh wa Wilaya ya Kahama, Alhaji Omary Damka, amewahusia vijana pamoja na wananchi kwa ujumla kuendelea kutunza amani na kuuishi utulivu katika majumba yao, maeneo ya kazi na katika shughuli zao za kila siku, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya mtu na jamii.

Akizungumza wakati wa tamasha la michezo lililofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Mhongolo wilayani Kahama, Shekh Damka amesema ushiriki wa wananchi katika michezo na shughuli za kijamii umewezekana kutokana na uwepo wa amani na utulivu. Ameeleza kuwa pasipo amani, hata shughuli za kijamii haziwezi kufanyika kwa ufanisi.

“Leo tumeweza kushiriki katika michezo hii kwa sababu ya amani na utulivu, Ingekuwa tarehe 29 Oktoba, sidhani kama kungekuwa na mtu hapa, Hivyo nawausia vijana, utulivu huu tulionao leo twendeni tukauishi katika majumba yetu, kazini, katika familia na kwenye shughuli zetu zote na amani ndiyo kila kitu; tukiwa na amani tutafanya mambo yetu vizuri na yataenda kama tunavyotaka,” amesema.

Aidha, Shekh Damka amepongeza mwenendo mzuri wa michezo hiyo akisema imechezwa kwa amani, nidhamu na ustaarabu mkubwa bila madhara kwa wachezaji.
“Hatujaona mtu kuvunjwa mguu, hivyo nawapongeza sana kwa mchezo mzuri na wa kistaarabu,” ameongeza.

Katika hatua nyingine, ameipongeza timu ya Juvikiba Madina kwa kuchukua kombe la ushindi, huku akiipongeza pia timu ya Juvikiba Mhongolo kwa kuonyesha ushindani mzuri na kucheza kwa kiwango cha kuridhisha.

Shekh Damka pia amebainisha kuwa ameweza kuteta jambo na, Mheshimiwa Diwani pamoja na Mtendaji wa Kata kuhusu kupanua wigo wa tamasha hilo ambapo amesema badala ya kushirikisha timu mbili pekee, tamasha linapaswa kushirikisha timu nyingi zaidi ili kuwepo na mechi za mtoano na hatimaye fainali kubwa.

“Tunataka kupanua wigo wa tamasha hili, lishirikishe timu mbalimbali, zipatikane mechi za mtoano na baadaye kuwe na fainali. Mimi mwenyewe nitaleta timu yangu ya Msikiti Mkuu wa Ijumaa, na naamini haitakuwa rahisi kuishinda,” amesema kwa utani wenye kuhamasisha.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mhongolo, Mheshimiwa Mariamu Sasi, ameunga mkono wito huo kwa kuahidi kushikamana na vijana wa kata hiyo na kuanzisha matamasha ya michezo ili kuimarisha mshikamano, umoja na amani.

Amesema vijana ni nguvu na tunu ya taifa, hivyo wanapaswa kulindwa kwa kudumisha amani, upendo na ushirikiano.
“Vijana ni nguvu na ni tunu ya taifa. Tuilinde tunu hii kwa kudumisha amani ambayo Mungu ametupa, kuwa na upendo na kushirikiana katika shughuli zetu za maendeleo,” amesema Diwani Mariamu Sasi.

Naye Diwani wa Kata ya Malunga Ahmed Haroun amesema yuko tayari kwenda kuhamasisha vijana wa kata yake ili wajitokeze kushiriki michezo na timu ya Mhongolo, akieleza kuwa lengo ni kujenga undugu, amani na mshikamano miongoni mwa vijana wa kata hizo.

Aidha, Mlezi wa timu ya Juvikiba Madina, Shekh Musini Juma, amesema matamasha kama hayo ni jukwaa muhimu la kuwatambulisha vijana wa dini ya Kiislamu kwa jamii pana, ili waweze kutumika katika dini kama wenzao waliowatangulia.

Ameeleza kuwa kupitia michezo, vijana wanaweza kuondolewa katika makundi hatarishi yanayojihusisha na vitendo viovu kama uvutaji wa bangi, wizi na maovu mengine, na hatimaye kurejeshwa katika misingi ya maadili mema kwa kushiriki shughuli za kidini, ikiwemo kuhudhuria misikiti.

Kwa upande wake, Kocha wa timu ya Juvikiba Mhongolo, Mrisho Ramadhani, amesema licha ya timu yake kupoteza mchezo kwa mikwaju ya penalti, tamasha hilo limefanikiwa kwa lengo lake kuu la kuwakutanisha vijana na kujenga mshikamano.

“Licha ya kufungwa kwa mikwaju ya penalti, bado tamasha hili limetuletea umoja. Tumejifunza, tumefurahi kushirikiana na wenzetu, na hilo ndilo jambo kubwa zaidi,” amesema Kocha Mrisho.

Tamasha hilo limeelezwa kuwa chachu ya kuimarisha afya, mshikamano na amani miongoni mwa vijana wa Wilaya ya Kahama, huku viongozi, makocha na wadau wakitoa wito kwa vijana kuendelea kuwa mabalozi wa amani na maadili mema katika jamii zao.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso