Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mbunge wa Jimbo la Peramiho, Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama, ambaye amefariki dunia leo.
Kupitia taarifa yake, Rais Samia amesema amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba huo mzito na kutoa pole kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, wananchi wa Jimbo la Peramiho, pamoja na familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, marehemu Jenista Mhagama alitoa mchango mkubwa kwa taifa katika kipindi cha zaidi ya miaka 38 akiwa mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Alitumika kama kiongozi wa vijana, kiongozi wa wanawake, na waziri katika serikali mbalimbali, akiacha alama kubwa katika siasa na uongozi nchini.
Rais Samia amemwelezea marehemu kama mnasihi na kiongozi aliyegusa maisha ya wengi, akisisitiza kuwa mchango wake utaendelea kukumbukwa daima.
“Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina,” amehitimisha Rais Samia.
— Mwisho —

No comments:
Post a Comment