MBUNGE NGAYIWA NA RC MHITA WAIAGIZA TANESCO KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Wednesday, 17 December 2025

MBUNGE NGAYIWA NA RC MHITA WAIAGIZA TANESCO KUBORESHA HUDUMA KWA WANANCHI


Mbunge wa Jimbo la Kahama, Mheshimiwa Benjamini Ngayiwa, akizungumza na Madiwani, wananchi pamoja na wataalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa lengo la kusikiliza na kujadili changamoto mbalimbali zinazohusu huduma ya umeme katika jimbo hilo.


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita (kushoto)akimkaribisha Meneja mpya wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Hadija Mbaruku ofisini kwake.

NEEMA NKUMBI NA MARCO MADUHU, KAHAMA SHINYANGA

Mbunge wa Jimbo la Kahama, Mheshimiwa Benjamini Ngayiwa, amekutana na madiwani, wananchi pamoja na wataalamu kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa lengo la kusikiliza na kujadili changamoto mbalimbali zinazohusu huduma ya umeme katika jimbo hilo.

Katika mkutano huo, wananchi na madiwani wameeleza kero zinazowakabili, ikiwemo ucheleweshaji wa kuunganishiwa umeme, gharama za uunganishaji pamoja na kukatika kwa umeme mara kwa mara bila taarifa ya awali.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Tito Kizozo, mkazi wa Kitwana, amemuomba Mbunge Ngayiwa kuwasaidia wananchi kupata huduma ya kuunganishiwa umeme kwa gharama ya shilingi elfu 27, akieleza kuwa gharama hiyo itawawezesha wananchi wengi kumudu na kupata huduma muhimu ya umeme kwa ajili ya maendeleo yao ya kijamii na kiuchumi.

Diwani wa kata ya Nyahanga Josephina Kilimba ameomba kuunganishiwa umeme katika mitaa ya Shunu na Lugera ambapo amesema kuwa katika maeneo mengi ya mitaa hiyo inahitaji huduma hiyo.


Kwa upande wake, Mbunge Ngayiwa amesisitiza umuhimu wa TANESCO kuboresha huduma zake na kuzingatia mahitaji ya wananchi, huku akiahidi kufuatilia kwa karibu changamoto zote zilizowasilishwa ili zipatiwe ufumbuzi wa haraka kwa kushirikiana na TANESCO na serikali za mitaa.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Shinyanga kuhakikisha linatoa huduma bora kwa wananchi, sambamba na kutoa taarifa kwa wakati pale linapofanya maboresho ya miundombinu ya umeme, badala ya kukata umeme ghafla.

Mhita ametoa maelekezo hayo leo Desemba 17, 2025, wakati akimkaribisha Meneja Mpya wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Hadija Mbaruku, aliyewasili ofisini kwake kujitambulisha rasmi.

Amesema licha ya TANESCO kufanya kazi nzuri ya kuboresha miundombinu ya umeme, bado changamoto kubwa imekuwa ni ukosefu wa taarifa kwa wananchi wakati wa maboresho hayo, hali inayosababisha kukatika kwa umeme ghafla na kuathiri shughuli za kiuchumi ikiwemo uzalishaji mali, hasa katika Wilaya ya Kahama.

“Karibu sana Meneja mpya wa TANESCO hapa mkoani Shinyanga, Maelekezo ya Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora,” amesema Mhita.

Aidha, amesisitiza TANESCO kuboresha kitengo chake cha mawasiliano na kutoa taarifa mapema kwa wananchi ili waweze kupanga ratiba zao kabla ya umeme kukatika, Ameeleza kuwa utoaji wa taarifa kwa wakati huimarisha mahusiano kati ya shirika na wananchi, akisisitiza kuwa “Information is power.”

Pia, Mkuu wa Mkoa ametoa maelekezo kwa TANESCO kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya umeme, pamoja na kusisitiza matumizi ya mafundi waliothibitishwa na TANESCO katika ufungaji wa mifumo ya umeme majumbani, ili kuepusha hitilafu na ajali za moto.

Mhita amepongeza pia uwepo wa Dawati la Malalamiko kwa ajili ya kupokea na kufuatilia kero za wananchi, akisisitiza kuwa utatuzi wa kero hizo kwa wakati huleta faraja na imani kwa wananchi.

Naye Meneja Mpya wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Hadija Mbaruku, ameshukuru kwa mapokezi mazuri na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote aliyoyapokea, ikiwemo kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Amesema maboresho ya miundombinu ya umeme yanatarajiwa kukamilika Desemba 23, 2025, na kubainisha kuwa TANESCO imeelekezwa kuhakikisha katika kipindi cha sikukuu za mwisho wa mwaka wananchi wanasherehekea bila usumbufu wa kukatika kwa umeme.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso