Kundi la vijana wachumi na wabunifu wa teknolojia wameibuka na kutoa wito kwa Serikali, wakisisitiza umuhimu wa Wizara ya Vijana kufanya kazi kwa karibu zaidi na Wizara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA). Wamesema kuwa katika zama za uchumi wa kidijitali, vijana wanahitaji nyenzo na ujuzi wa kiteknolojia ili kuweza kushindana na kunufaika na fursa zilizopo.
Kauli hiyo imetolewa na mmoja wa vijana ambaye yuko mwaka wa pili Chuo Kikuu akijifunza Uhandishi, Mashilingi Raphael katika mahojiano kuhusu uwapo wa wizara hiyo mpya inayoenda kushughulika na masuala ya vijana.
"Uchumi wa dunia kwa sasa hauwezi kutenganishwa na teknolojia. Kila kitu, kuanzia kilimo hadi biashara, kinategemea data, app na mifumo ya kidijitali hivyo ni muhimu sana kwa wizara hizi mbili kuwa na desk la pamoja kuwasaidia vijana." alisema Mashilingi.
"Tunaishukuru Serikali kwa kuwekeza katika miundombinu ya intaneti, lakini ni wakati sasa Wizara ya Vijana iwekeze kwa vijana kwa kuwapa ujuzi wa TEHAMA unaolingana na fursa hizi. Haitoshi kusema 'ajira zipo'; tunahitaji kujua jinsi ya kuzifikia ajira hizo kupitia simu zetu na kompyuta," alisema Bi. Aisha Mtiro mjasiriamali soko la ndizi Mabibo.
Kijana mwingine, Bw. Eliya Kobero, mtaalamu wa utengenezaji wa programu (software developer), alielezea kuwa ushirikiano huo unapaswa kuanza kwa kuunda programu za mafunzo (training programs) zinazoongozwa na Wizara ya Vijana lakini zikitekelezwa na wataalamu wa Wizara ya TEHAMA.
Aidha alishauri kuundwa kwa Mfumo wa Mtandaoni (Platform) wa taifa, ambao utatumiwa na Wizara ya Vijana kutangaza fursa za mikopo, mafunzo ya ufundi, na nafasi za ajira zinazohitaji ujuzi wa kidijitali. Pia mtandao huo utatambulisha mafunzo ya kanuni za programu (Coding) na kuleta karibu startup za vijana na wawekezaji kupitia majukwaa ya kidijitali yatakayosimamiwa kwa pamoja.
Wazungumzaji waliongeza kuwa bado kuna pengo kubwa kati ya ujuzi wa vijana wengi na mahitaji ya soko la ajira la kidijitali.
"Kampuni zinahitaji watu wenye ujuzi wa Digital Marketing, Data Analysis, na Cybersecurity. Hizi sio kazi za kawaida tena; hizi ndio kazi za kesho," alieleza Bw. Eliya.
"Tunahitaji Wizara ya Vijana ifanye kazi na Wizara ya TEHAMA kuhakikisha vijana wanapata vyeti vinavyotambulika vya ujuzi huu, na sio tu vyeti vya 'kozi fupi' za kompyuta."
Katika kuzingatia mahitaji halisi ya sasa na baadae Rais Samia akitumia malaka yake aliunda wizara ya vijana na kuagiza kuhakikisha inatatua changamoto zao ikiwepo kuweka mazingira mazuri ya vijana kuajiri na kuajiriwa.

No comments:
Post a Comment