Mkuu wa Wilaya ya Kahama Frank Nkinda, ameongoza kikao maalum na Viongozi wa Dini pamoja na wajumbe wa Baraza la Amani Wilaya ya Kahama, chenye lengo la kujadili hali ya amani na kuweka mikakati ya kuendelea kuilinda amani katika wilaya hiyo.
Kikao hicho kimefanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, kikihusisha viongozi kutoka madhehebu mbalimbali ya kidini ambao wamekutana kubadilishana mawazo juu ya namna bora ya kudumisha maelewano, mshikamano na utulivu wa jamii.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Dc Nkinda amesisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa ustawi wa wananchi na maendeleo ya wilaya, akibainisha kuwa Serikali inaiona nafasi ya viongozi wa dini kama ya msingi katika kuhamasisha maadili, uwajibikaji na utulivu wa kijamii.
"Kahama imekuwa mfano wa maeneo yenye utulivu na mshikamano, Ili tufike mbali zaidi, tunahitaji ushirikiano wa dhati kati ya Serikali na taasisi za dini, Amani haitokei tu tunaitengeneza na kuilinda kwa pamoja", amesema Mhe. Nkinda.
Kwa upande wao, viongozi wa dini wameipongeza Serikali kwa utaratibu wa kuwaleta pamoja na kuwashirikisha katika masuala muhimu yanayoigusa jamii, huku wakiahidi kuendelea kuwa mstari wa mbele kuhimiza amani, upendo na uvumilivu miongoni mwa waumini na wananchi kwa ujumla.
Baraza la Amani limesema kuwa litaendeleza majadiliano na mikutano ya mara kwa mara ili kuhakikisha changamoto ndogo ndogo zinazoweza kuhatarisha amani zinatambuliwa mapema na kutafutiwa suluhu.
Kikao hicho kimehitimishwa kwa makubaliano ya kuongeza ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za dini na wadau wengine, kuhakikisha Kahama inasalia kuwa wilaya salama, yenye utulivu na mwelekeo mzuri wa maendeleo.






No comments:
Post a Comment