
Serikali ya Awamu ya Sita imesisitiza kuwa Watanzania hawana sababu yoyote ya kuitikia miito ya vurugu na maandamano, kwani tayari Tume ya Uchunguzi iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan ndiyo jukwaa rasmi na la kisheria la kushughulikia kiini cha vurugu za Oktoba 29, 2025. Huku Serikali ikisisitiza kazi ya Tume, viongozi wa dini wameonya kuwa matukio ya vurugu za awali yatoe funzo la kutosha kwa taifa.
Serikali imeeleza wazi kuwa Tume hiyo, inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othmani, imesheheni mamlaka ya kuchunguza mambo mawili makuu yenye utata:Chanzo cha Fedha: Kutafuta kwa kina fedha walizolipwa vijana waandamanaji walioshiriki kwenye vurugu na ushiriki wa Taasisi Zisizo za Serikali (NGO), za ndani na za nje, zilizochangia katika kufadhili vurugu hizo.
Madhumuni makuu ya Rais Samia ni Tume "kutafuta majibu ya kitaalamu kwa maswali haya ili kulinda vijana na rasilimali za nchi."
Kwa kuwa Serikali imechukua jukumu hili la msingi, wananchi wote, hususan vijana, wanatakiwa kuepuka kabisa miito yoyote ya maandamano au vurugu inayoenezwa mitandaoni, kwani hoja za msingi zenye utata sasa ziko chini ya uchunguzi wa kitaifa.
Kauli ya Serikali imeungwa mkono na viongozi wa dini, ambao wamewataka waumini wote kuepuka vitendo vinavyoweza kusababisha machafuko.
Bw. Sherally Hussein Sherally, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Msikiti wa Al Jumaa jijini Mwanza, amesema matukio ya Oktoba 29 yametoa funzo muhimu kwa taifa, akionya kuwa vurugu hizo zilitokana na baadhi ya watu kudhania kuwa ni masuala madogo, ilihali matokeo yake yalikuwa makubwa.
“Sisi kama Waislamu tunapinga vikali hatua zozote au maneno yoyote au taasisi yoyote au chama chochote ambacho kina malengo ya kuleta vurugu katika nchi hii,” alisema Bw. Sherally akisisitiza, “Vurugu zilizotokea Oktoba 29 zimetupa funzo, na kuna wakati tulidhania ni masihara lakini hayakuwa masihara tumeona matokeo yake.”
Bw. Sherally pia alitoa onyo kali kuhusu taarifa zinazodai kuwepo kwa makundi yanayopanga kuandamana Desemba 9, akieleza kuwa siku hiyo ni maalumu kwa maadhimisho ya Uhuru wa Tanganyika, hivyo haipaswi kuchanganywa na masuala ya vurugu.
“Kwahiyo Desemba 9 kujitokeza kwa kile wanachokitaka kufikisha ujumbe wanaoutaka sio siku yake, hiyo ni siku ya sherehe, tunataka kusherekea uhuru wa Tanganyika, tusiingiziwe kitu mbadala wa sherehe tulizokuwa tumeandaa,” alisema Bw. Sherally.
Wito wa Serikali na viongozi wa dini unasisitiza kuwa suluhisho la changamoto za kisiasa sasa lipo chini ya uchunguzi wa Tume, na ni wajibu wa kila Mtanzania kutoa nafasi kwa Tume hiyo ya kisheria kufanya kazi yake badala ya kuanzisha vurugu mpya.
@@@@@@@@@@@@
Serikali inavyokamata fundo la maadui wa Tanzania kupitia Tume na BoT
Wakati Jamii ya Kimataifa ikielekeza nguvu kwenye kuripoti vurugu zilizotokea nchini, uongozi wa dini na Serikali umebainisha kuwa matukio haya ni sehemu ya ajenda kubwa na ovu ya vita vya kiuchumi inayoendeshwa mtandaoni kwa lengo la kudumaza Taifa.
Hatua za Serikali, ikiwemo kuunda Tume ya Uchunguzi na kauli za Benki Kuu, zimekuwa jibu la moja kwa moja la kukabiliana na mkakati huu.
Sheikh Pembe Ahoji Nia ya Vyombo vya Nje
Sheikh Shaban Pembe, Imamu wa Msikiti wa Mtambani, amehoji nguvu kubwa iliyowekwa na vyombo vya habari vya kimataifa (kama CNN na BBC) na baadhi ya nchi jirani (hususan Kenya) kuripoti matukio ya vurugu yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
"Amehoji kama ni huruma ya dhati kwa Tanzania, au kama kuna 'ajenda iliyojificha nyuma ya mwamvuli wa haki,'" alisema Sheikh Pembe.
Sheikh huyo alidai kuwa miaka ya nyuma Kenya ilitegemea soko la Tanzania, lakini sasa uzalishaji wa ndani umeongezeka na bidhaa nyingi zina nembo ya ‘Made in Tanzania’, akionesha kuwa ushindani wa kiuchumi unaweza kuwa chanzo cha maslahi ya kibatili.
Mkakati wa Serikali: Tume na BoT Zakamata Fundo
Serikali imejibu vita hivi vya mtandaoni kwa hatua za kisheria na kiuchumi, zikilenga kutafuta kiini cha fedha na upotoshaji:
Tume ya Uchunguzi :
Serikali imeunda Tume ya Uchunguzi inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu Mohamed Chande Othmani kuchunguza madai ya fedha walizolipwa vijana waandamanaji na kufichua ushiriki wa Taasisi Zisizo za Serikali (NGO) za ndani na nje.
Serikali imesisitiza kuwa Tume hii ndiyo "jukwaa rasmi na la kisheria" la kutafuta majibu ya kitaalamu kwa maswali haya, ikiwa ni hatua ya moja kwa moja ya kukabiliana na agenda zilizofichwa.
Benki Kuu Yapinga Vita vya Mifumo ya Fedha:
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imelazimika kutoa taarifa ya umma kufuatia uzushi ulioenezwa mtandaoni kudai kuwa mifumo ya benki haiko salama. Lengo la uzushi huu ni kuwatia hofu wananchi, kuwaondoa amana zao, na kudhoofisha mtaji wa benki.
Gavana Emmanuel M. Tutuba alikanusha vikali, akithibitisha kuwa mifumo ya malipo ya Taifa iko "salama na inaendelea kuzisimamia kwa ufanisi". BoT iliwaonya wote wanaoeneza upotoshaji huo watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Wito kwa Uzalendo
Kwa hatua hizi, Serikali inatoa ujumbe kuwa vita vya kiuchumi na uchochezi wa mtandaoni havitavumiliwa. Wito unatolewa kwa Watanzania kukataa miito ya maandamano na vurugu, kuamini taasisi zao za kibenki, na kupuuza taarifa za uongo ili kulinda utulivu wa kiuchumi na amani ya Taifa.
@@@@@@@@@@
Kero ya maandamano na msongo wa mawazo: Wito wa Kuachana na 'Drama' Zinazowatesa Walala Hoi
Kufuatia matukio ya ghasia na machafuko yaliyotokea nchini kufuatia hali ya kisiasa, wananchi wengi wamejikuta katika hali ya ongezeko la msongo wa mawazo (stress) na hofu kubwa. Wataalamu wa saikolojia wanaonya kuwa kitendo hiki kimeacha makovu ya kina na kinaendelea kusababisha madhara ya kiafya ya akili kwa Watanzania, hasa wale wa kipato cha chini.
Akizungumza , Mwanasaikolojia na Mkurugenzi wa Shirika la Rafiki wa Watoto (RAWATO), Peter Manyama, alieleza kuwa matukio ya vurugu yanazalisha hofu, wasiwasi, na uchungu mkubwa miongoni mwa jamii.
Akifafanua zaidi alisema:" Kuna hasara za Kimaisha: Watu wamepoteza ndugu, mali, kazi, na wengine wamejikuta kwenye deni la mikopo bila uwezo wa kulipa. Lakini pia kuna Hofu na Machungu: Maneno, picha, na kumbukumbu za vurugu zilizopita huacha historia mbaya katika akili za watu na kujenga hali ya kutoelewana hasa kwa taarifa zinazoendelea kuhusu vitisho vya kurudiwa kwa vurugu. Kama vile wito wa ‘Tarehe 9’, zinawavuruga zaidi Watanzania kwa kujiuliza, Je, kitakuwa kikubwa zaidi ya kilichopita au kidogo?"
Manyama anatahadharisha kuwa hali hii ikiachwa bila hatua za mapema, itasababisha watu wengi kuingia katika matatizo makubwa ya afya ya akili. Mmoja wa wanamitandao aliandika katika posti yake kwamba: "Mimi mpaka leo usingizi napata kwa shida sana, kila nikilala nahisi kama kuna mtu ananiamsha ."
Kataa 'Drama' Zinazonufaisha Wenye Pesa
Kutokana na maoni kutoka mtaani, kuna kilio kikubwa cha kuomba viongozi na waandaaji wa matukio ya kisiasa kuacha 'drama' hizi za maandamano, kwani zinaonekana kuwanufaisha wale wenye fedha na ajenda maalum, huku zikiwatesa na kuwarudisha nyuma wananchi wa kawaida.
"Maisha ya kweli huku mtaani ambako ndio kuna maisha halisi achana na haya maisha ya mtandaoni huku watu wamechoka na hizi drama... hizi drama ziliwarudisha nyuma watafutaji wengi ziliwapa hasara, ziliharibu muda wao wa thamani. Mtaani watu hawahitaji haya maandamano yenu."
Watu wa kipato cha chini, ambao wanategemea kazi zao za kila siku, ndio hupata hasara kubwa kunapotokea vurugu kwani ghasia hizo husimamisha biashara na shughuli za kila siku, hivyo kuwanyima walala hoi mapato ya kuendesha maisha.
Kuna madai kuwa waandamanaji wengi huandaliwa, kulipwa, na kupewa mafunzo, huku wakitamani kurubuni asilimia kubwa ya vijana wa mitaani ambao baada ya Oktiba 29 wametambua balaa la kujiingiza katika vurugu.
Hatua Zinazopaswa Kuchukuliwa
Wataalamu na wananchi wanatoa wito wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka ambapo wazazi na walezi wanatakiwa kuwajibika kikamilifu kuwalinda watoto na vijana wao dhidi ya kujiingiza kwenye vurugu au kuchochewa na wanasiasa.
Aidha Jumuiya za dini (Makanisa na Misikiti) na taasisi zingine za kijamii zinapaswa kuweka kipaumbele katika kuwajenga kisaikolojia waumini na wananchi wao ambao wameathirika na msongo wa mawazo na kupoteza mali huku wakizuia au kupunguza matamshi na vitendo vinavyoweza kuibua upya machafuko, kwa faida ya amani na ustawi wa kila Mtanzania.
No comments:
Post a Comment