Jeshi la Polisi nchini limeendeleza kampeni ya kutoa elimu na kuimarisha ushirikiano na wananchi katika mikoa mbalimbali, likisisitiza umuhimu wa jamii kuwa walinzi wa amani na kufichua mapema viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani, ikiwemo kuwafichua wageni na watu wenye nia mbaya.
Viongozi wa Polisi kutoka Mikoa ya Njombe, Katavi, na Tanga wametoa wito kwa makundi tofauti, kuanzia Maafisa Usafirishaji (Bodaboda), Wafanyabiashara, Vijana, hadi Wafugaji, kuweka kipaumbele katika kulinda amani, kwani ndiyo msingi wa maendeleo na mafanikio ya Taifa.
Bodaboda Waaswa Kufichua Wageni na Kuwajibika Mtandaoni
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Mahamoud Hassan Banga, amewataka Maafisa Usafirishaji kutumia Mitandao ya Kijamii kwa busara na si kwa uchochezi au uvunjifu wa amani.
Akiwasihi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi, Kamanda Banga ametoa wito maalum kwa Bodaboda kuacha kuwasafirisha au kuwaficha watu wenye nia ovu na nchi , hasa wale wanaotaka kuvuruga amani. Badala yake, wametakiwa kushirikiana na Polisi kuwafichua watu wote hawa, ikiwemo wageni, ili hatua stahiki zichukuliwe mapema.
Puuzeni Wachochezi wa Mitandaoni na Epukeni Kurubuniwa
Kwa upande wa Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa, Mrakibu wa Polisi (SP) John Mwaipungu, amewataka wananchi kuwapuuza na kuwakemea kwa nguvu zote wale wote wanaohamasisha vitendo vya uvunjifu wa amani kupitia Mitandao ya Kijamii.
SP Mwaipungu ameeleza kuwa vitendo vya uchochezi ni kosa kisheria na vinatoka kwa watu wasio na mapenzi mema na nchi yao. Aidha, amewaonya vijana kutokukubali kurubuniwa na kujiingiza katika uhalifu, akisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika.
Toa Taarifa Mapema: Ushirikiano ni Nguzo Muhimu
Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga limeendeleza jukumu la kutoa elimu kwa jamii. Mratibu wa Polisi Jamii Wilaya ya Lushoto, SP Emanuel Shilla, alipokutana na wafanyabiashara, alisisitiza umuhimu wa kutoa taarifa mapema za viashiria vyovyote vya uchochezi au uvunjifu wa amani.
SP Shilla alieleza kuwa ushirikiano kati ya jamii na Jeshi la Polisi ndio nguzo kuu ya kuimarisha usalama na kuzuia matukio kabla hayajatokea. Wananchi wa Lushoto wameahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa kutoa taarifa sahihi na za wakati.
Wakati huohuo, katika Wilaya ya Handeni, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Tanga, ACP Wambura, alikutana na Wafugaji wa jamii ya Kimasai na kuwasihi kuepuka migogoro na kuwa mabalozi wa amani kwa kutoa taarifa za uchochezi au vurugu mara wanapozibaini.
Polisi inahimiza wananchi:
Amani ni Mtaji Wetu Mkuu. Kwa kila Mtanzania kuacha kurubuniwa, kupuuza ‘drama’ zinazonufaisha watu wachache, na kutoa taarifa za viashiria vya uvunjifu wa amani, tutakuwa tumelinda maendeleo yetu binafsi na Taifa kwa ujumla. Tumia namba za dharura za Jeshi la Polisi kutoa taarifa zako kwa usiri na usalama.

No comments:
Post a Comment