Somo la Uchungu: Baada ya Oktoba 29, Vijana Waonya Dhidi ya Uchochezi wa Desemba 9
Katika hali inayoonyesha jinsi amani ilivyo kiungo muhimu cha maisha ya kila siku, vijana wanaoishi maeneo yaliyokumbwa na vurugu za hivi karibuni wamejitokeza na kutoa ushuhuda wao mzito.
Abdallah Vincent Machali, akizungumza kwa uchungu, alielezea madhara makubwa yaliyoambatana na vurugu za Oktoba 29, akisisitiza kuwa madhila yaliyotokea hayana ulinganifu na chaguzi au matukio mengine aliyopitia hapo awali.
“Jambo hili limetuathiri kwa kiasi kikubwa sana kwa sababu huduma za chakula zilikosekana. Mkate ule uliadimika kwelikweli. Ukienda sokoni kama unataka nyanya, huwezi kuipata, wala chochote ambacho kilikuwa kama huduma kwa jamii kilikuwa hakuna.”
Machali alibainisha kuwa madhara hayo hayakuathiri sekta moja tu, bali sekta zote, ikiwemo sekta ya wanafunzi na huduma muhimu za kijamii. Hii inathibitisha kuwa hakuna maisha bila amani.
Machali anasema baada ya kushuhudia pigo hili kubwa, anaamini kwamba somo lililopatikana ni la kudumu, na litaondoa kabisa shauku ya vijana kujiingiza tena kwenye vurugu.
"Kuna pigo moja kubwa, kila mmoja kajifunza. Kwa hiyo sidhani tena kuwa kutatokea tena jambo kama hilo... Sidhani kama kuna kijana mwenye akili timamu nchini atajitokeza tena kufanya vurugu Desemba 9."
Alisisitiza wito wake kwa vijana wenzake na wananchi wote: "Tujitahidi sana kuwa makini na maneno ya kiuchochezi au maneno yanayoweza kusababisha amani kutoweka. Vita usikie kwa majirani, sio kwenu."
Maoni ya jumla kutoka kwa wananchi yanaunga mkono wito wa amani na utulivu, huku wakimkumbatia Rais Samia Suluhu Hassan na dhana ya mazungumzo kama msingi wa uponyaji wa jamii.Aidha Wananchi wanasisitiza kwamba amani ni tunu na fahari kubwa sana, na ni fursa ya maendeleo, na hivyo inapaswa kulindwa kwa nguvu zote.
Wito wa "Tunampenda Mama, Tunataka Amani" unaosambaa mitandaoni unaonyesha utayari wa jamii kumpa Rais Samia nguvu ili aweze kuleta maendeleo, huku wakisisitiza kuwa mazungumzo ndio msingi, na kwamba sisi ni Taifa moja.
Ushuhuda wa Abdallah Machali na maoni ya wananchi ni funzo kubwa: amani ndiyo uhai wa biashara, chakula, elimu, na ibada. Baada ya kushuhudia uchungu wa kukosekana kwa huduma, inaaminika kuwa hakuna kijana atayetaka kurudi kwenye giza. Tukemee kila dalili ya chuki na kulinda urithi huu kwa nguvu zote.

No comments:
Post a Comment