
Aliyekuwa nguli wa siasa za upinzani na Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria (Kanda ya Ziwa) wa Chadema, Ndugu Ezekia Wenje, amesisitiza kuwa uamuzi wake wa kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM) haupaswi kuchukuliwa kama kitendo cha usaliti, bali ni uamuzi wa uzalendo wa kimkakati wa kutafuta eneo bora la kufanyia siasa kwa maendeleo ya wananchi.
Akizungumza kwa hisia kali wilayani Muleba, mkoani Kagera, wakati wa mkutano wa kampeni wa Mgombea Urais wa CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, Wenje alibainisha kuwa CCM ndicho chama kinachompa fursa kiongozi kushiriki moja kwa moja katika kutatua changamoto za wananchi na kusukuma mbele ajenda za maendeleo ya Taifa.
Wenje, ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Nyamagana na mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, alifichua wazi sababu kuu za chama hicho kususia Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akieleza kuwa chama hicho kimepoteza mwelekeo na kufilisika kisiasa.
Alisema, uamuzi wa kususia Uchaguzi Mkuu unaonyesha wazi ukosefu wa mshikamano na udhaifu mkubwa wa chama hicho kisiasa. Wenje alibainisha kuwa migogoro ya muda mrefu, hasa mivutano baina ya viongozi wake wakuu (akiitaja Team Mbowe na Team Lissu), imevuruga misingi ya chama, kuharibu umoja, na kuwavunja moyo maelfu ya wanachama, na hivyo kusababisha Chadema kutokuwa na nguvu za kushindana kihalali.
"Ukiona kiongozi wa Chadema anasema yuko tayari kwa lolote, ujue amekata tamaa. Kazi ya kiongozi ni kuonesha njia, si kukatisha tamaa wafuasi wake," alisema Wenje kwa msisitizo, akisisitiza kuwa chama hicho kimegeuka kuwa chombo cha misukumo ya wanaharakati wanaofadhiliwa na taasisi za kimataifa, badala ya kuwa chama cha kisiasa kinacholenga kuunda sera.
Wenje alihitimisha kwa kusisitiza, "CCM ni chama chenye mfumo, maono na dira. Ndiyo maana nimeondoka kwenye siasa za mchangani na kurudi hapa kushiriki katika kazi ya kweli ya kujenga Taifa, kwa kushirikiana na Dkt. Samia Suluhu Hassan na chama chake."
No comments:
Post a Comment