WAPONGEZA AZIMIO LA VIONGOZI WA VYOMBO VYA HABARI. - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Sunday, 26 October 2025

WAPONGEZA AZIMIO LA VIONGOZI WA VYOMBO VYA HABARI.




Na Mwandishi Wetu


Kwa mara ya kwanza katika historia ya karibuni ya uchaguzi, wakuu wa vyombo vya habari na wahariri wameungana na kutoa azimio la pamoja, wakihimiza wananchi wote kutanguliza amani na utulivu kabla na baada ya uchaguzi mkuu. Azimio hili linaambatana na wito wa kukataa "uwenda wazimu wa halaiki" unaoweza kutumiwa na wachache kubomoa misingi ya kitaifa iliyojengwa kwa miaka mingi.



Wadau hao wanasisitiza kwamba njia pekee ya kulinda amani na kujenga taifa imara ni kupitia ushiriki mkubwa na wa amani wa wananchi katika zoezi la upigaji kura.


Azimio hilo linasisitiza kuwa uchaguzi ni daraja la kuimarisha demokrasia, na si uwanja wa vita.


"Ushiriki mkubwa wa wananchi huimarisha misingi ya demokrasia nchini. Ni haki yako ya msingi ya kikatiba. Kwa kutekeleza haki hii, unasaidia kujenga utawala bora ambapo sauti ya kila mwananchi inathaminiwa," inasema sehemu ya azimio hilo.




Vyombo vya habari vinawahimiza Watanzania kuchukua hatua hii kama fursa ya kutumia haki yao ya kikatiba badala ya kutoa nafasi kwa vurugu au uchochezi. Kupiga kura kwa amani ni kuzuia kabisa jaribio lolote la kuharibu utulivu wa nchi.


Kataa Kubomoa Misingi ya Kitaifa

Wahariri wameeleza wasiwasi wao kuhusu baadhi ya sauti zinazoweza kutumika kusukuma ajenda ya uvunjifu wa amani kwa maslahi binafsi.


"Tunawaomba wananchi wasikubali kuingia katika uwenda wazimu wa halaiki na kubomoa misingi ya kitaifa. Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuwa Balozi wa Amani kuanzia kituo cha kupigia kura hadi anaporudi nyumbani," inahimiza taarifa hiyo.


Vyombo vya habari vimeahidi kuendelea kutoa taarifa sahihi na za kuelimisha, huku vikisisitiza kwamba utawala bora unajengwa na wananchi wenye utashi wa kwenda kwenye sanduku la kura. Kila mpiga kura anapaswa kujitambua kuwa yeye ni sehemu ya ulinzi wa amani ya nchi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso