Hekima ya Kauli: Kutenganisha Matukio ya Hapa na Pale na Utendaji wa Dola
Na Mwandishi Wetu
Katika hali ya kuelekea Uchaguzi Mkuu, ni muhimu sana kwa viongozi wa dini na wanasiasa kutumia lugha yenye hekima na busara ili kulinda amani na utulivu wa nchi.
Kutoa kauli zinazotafsiri matukio ya hapa na pale (Isolated Incidents) kama ishara ya Serikali kushindwa kulinda raia wake si sahihi, hasa wakati maisha ya Watanzania yanaendelea kwa amani na shughuli zote za kiuchumi kuabudu na kisiasa zikifanyika bila bughudha.
Wajibu Mkuu wa Serikali na Uhalisia wa Dunia
Jukumu kuu (Prime Task) la Serikali yoyote duniani ni kulinda raia wake na mali zao. Tanzania inatekeleza jukumu hili kwa ufanisi mkubwa. Ni kweli kwamba, kama ilivyo katika mataifa mengine duniani—hata yale yenye nguvu kubwa za kiulinzi—matukio ya kupotea kwa watu au uhalifu hutokea. Haya ni Matukio ya Kusikitisha, ya hapa na pale lakini hayapaswi kutafsiriwa kama Serikali imeshindwa kutimiza wajibu wake.
Ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania inaendelea kuwa Kisiwa cha Amani katika ukanda wa Afrika Mashariki, ikihifadhi maelfu ya wakimbizi kutoka mataifa jirani yanayokabiliwa na machafuko, kutokana na utulivu wake wa kiusalama.
Tahadhari kwa Viongozi wa Dini: Busara ya Kisera Inahitajika
Viongozi wa dini wamekuwa nguzo muhimu katika kulinda maadili na kuhimiza amani. Hata hivyo, mahubiri au matamko yanayotolewa lazima yazingatie uhalisia wa jamii na busara ya kisera, vinginevyo yanaweza kusababisha taharuki isiyo ya lazima na kupoteza imani ya waumini.
Kwa heshima kubwa kwa Taasisi ya Kanisa Katoliki na mchango wa uongozi wake, ni muhimu kutambua kwamba amani na utulivu tulionao leo nchini ni matokeo ya uwajibikaji wa Serikali kwa neema ya Mungu, na si kwa bahati au uzembe wa taasisi za dola.
Hoja ya msingi ni hii: Kauli kwamba Serikali haijatekeleza jukumu la kuwalinda raia wake si sahihi. Hii inathibitishwa na ukweli kwamba Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam linaendesha miradi mingi ya huduma na biashara (ikiwemo shule, hospitali, na taasisi za misaada). Je, kuna mradi wowote wa Kanisa uliosimama kwa sababu ya hali ya usalama nchini? Jibu ni hapana.
Kutenganisha Siasa na Imani
Ni muhimu kukumbusha kwamba ndani ya Kanisa Katoliki kuna waumini wenye mitazamo tofauti ya kisiasa. Si sahihi kuchukua hoja au malalamiko ya chama kimoja cha siasa, au matamanio binafsi ya viongozi wa kiroho, na kuyaweka kama sauti ya raia wote.
Viongozi wa dini wanapaswa kuepuka kuzungumza kwa mtazamo wa kisiasa unaoweza kuwagawa waumini wao wenye imani moja lakini itikadi tofauti. Matukio ya baadhi ya viongozi wa dini kuhusishwa moja kwa moja na ajenda za kisiasa huhatarisha umoja wa waumini.
Jukumu la Vyombo vya Dola
Serikali kupitia Jeshi la Polisi imechukua hatua za kiusalama pale inapobidi. Vyombo vya dola vimekuwa vikifuatilia kwa ukaribu kila tukio linalohusiana na amani na usalama wa raia, vikifanya uchunguzi kwa mujibu wa sheria.
Kuna ukweli kwamba matukio mengine ya kupotea au kutekwa yamebainika kuwa na sababu za kifamilia, kisaikolojia, au kibiashara (kama ilivyojitokeza kwa baadhi ya matukio yaliyoripotiwa), lakini vyombo vya dola vimekuwa vikishughulikia kila tukio kwa umakini na uwajibikaji. Intelligence ya Serikali ni kubwa, na inaendelea kufanya kazi kwa masaa 24 kwa siku kuhakikisha wananchi na mali zao zipo salama.
Amani ni urithi na wajibu wa pamoja. Viongozi wa dini wanapaswa kusaidia kulinda hali hii ya utulivu badala ya kutoa matamko yanayoweza kuibua tafsiri potofu au kuondoa imani kwa vyombo vya dola vinavyofanya kazi usiku na mchana.
No comments:
Post a Comment