
Neema Nkumbi, Kahama
Mkuu wa wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, ameipongeza Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa hatua ya kuzindua dawati maalumu kwa ajili ya wafanyabiashara, hususan wale wanaofanya shughuli zao katika sekta isiyo rasmi, akisema ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika viwanja vya TRA Kahama wakati wa uzinduzi huo, DC Nkinda amesema dawati hilo litasaidia kujenga mahusiano bora kati ya serikali na wafanyabiashara, sambamba na kuendeleza huduma bora kwa ustawi wa wananchi.
“Kupitia dawati hili mtajenga mahusiano mazuri na kuhakikisha biashara zinakua, TRA mkaishi katika dhima ya kutoa huduma bora kwa ustawi wa wanakahama, Naendelea kuipongeza TRA kwa kasi kubwa ya ukusanyaji wa mapato, wananchi wanataka huduma bora hivyo tunawategemea sana. Endeleeni pia kusisitiza wafanyabiashara kutoa risiti,” amesema Nkinda.
Kwa upande wake, Meneja wa TRA mkoa wa kikodi Kahama, Siwaka Kamwamu, amesema sekta isiyo rasmi ina umuhimu mkubwa katika uchumi wa taifa kwa kuwa inatoa ajira kwa zaidi ya watu milioni saba na kuchangia zaidi ya asilimia 30 ya pato la taifa.
Ameongeza kuwa bado wafanyabiashara wadogo wanakumbana na changamoto nyingi ikiwemo kutokurasimishwa kwa biashara zao na kutopewa nafasi ya kutambulika na taasisi mbalimbali, zikiwemo taasisi za kifedha.
Kamwamu amesema dawati hilo litakuwa daraja la kuwasikiliza, kuwaelimisha na kuwawezesha wafanyabiashara wadogo, sambamba na kutatua changamoto zao zinazohusiana na usajili na masuala ya kikodi.
“Dawati hili litawasaidia wafanyabiashara kufuata taratibu za usajili, kuwasilisha kodi kwa wakati, kupata huduma bora na kujenga mahusiano ya karibu kati yao na TRA Pia litafuata maadili ya msingi ya uweledi, uwajibikaji, uadilifu na uaminifu,” amesema Kamwamu.
Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara Kahama, Charles Machali, ameishukuru TRA kwa kuzindua dawati hilo akisema sasa wafanyabiashara ni marafiki wa serikali huku akiongeza kuwa hatua hiyo inaleta matumaini ya mazingira bora ya biashara pia akiwataka wenzake kushirikiana kikamilifu na TRA kwa kulipa kodi.
“Tunatamani mazingira ya biashara na serikali yaboreshwe zaidi, Wafanyabiashara sasa ni marafiki na serikali, tunaomba wilaya yetu iendelee kuimarisha mshikamano huu,” amesema Machali.
Uzinduzi wa dawati hilo unatajwa kuwa kiunganishi muhimu kati ya serikali na wafanyabiashara kwa lengo la kuongeza tija katika ukusanyaji wa kodi, kurahisisha utoaji wa elimu ya kodi na kuimarisha uchumi wa wananchi wa Kahama na taifa kwa ujumla.
No comments:
Post a Comment