CCM YAZINDUA KAMPENI JIMBO LA USHETU, CHEREHANI ANADIWA KWA WANANCHI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 13 September 2025

CCM YAZINDUA KAMPENI JIMBO LA USHETU, CHEREHANI ANADIWA KWA WANANCHI


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa akizungumza na wananchi wa ushetu katika Uzinduzi wa kampeni katika jimbo hilo.


Na Neema Nkumbi - Huheso digital Ushetu Kahama


Chama cha Mapinduzi (CCM) leo kimezindua rasmi kampeni zake za uchaguzi katika Jimbo la Ushetu, kikimnadi mgombea wake wa ubunge Emanuel Cherehani, katika mkutano uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Ilamba, Kata ya Igwamanoni.


Uzinduzi huo umeongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, ambapo ameyewataka wananchi kumpa kura mgombea huyo pamoja na Rais Samia na madiwani wa chama hicho.


Mlolwa amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeleta maendeleo makubwa katika jimbo hilo ikiwemo miradi ya maji kutoka Ziwa Viktoria, ujenzi wa madaraja yaliyokuwa yameshindikana, pamoja na miradi ya barabara.


"Tunapokuja kwenu tunakuja na hoja za msingi, kura nyingi zielekezwe kwa rais, wabunge na madiwani wa CCM," amesema Mlolwa.


Kwa upande wake, mgombea ubunge Cherehani ameahidi kutetea maslahi ya wakulima na wajasiriamali, kuongeza madarasa katika shule ya Sunga, pamoja na kushughulikia changamoto za wafugaji kwa kuwapatia maeneo maalum ya malisho yasiyokuwa na usumbufu wa askari wa hifadhi.


Cherehani ameahidi kuboresha miundombinu ya barabara za moramu zinazounganisha kila kata, na kuendeleza mji wa Kahama kwa kiwango kipya cha maendeleo. "Tunazitaka kura zote ziwe kwenye sanduku, wananchi wa Ushetu waendelee kutuamini kwa kazi na si kwa maneno," amesema.


Wananchi walioshiriki uzinduzi huo walitoa maoni yao kuhusu mahitaji ya jimbo, Zakaria Kisheza, mkazi wa eneo hilo, amewataka viongozi watakaochaguliwa kuhakikisha miundombinu ya barabara, maji na hospitali inaboreshwa


Mwananchi mwingine Fortunata Emanuel, ameomba viongozi wapya kuwasaidia kupata mikopo kwa urahisi na kujenga shule karibu na vijiji, akibainisha kuwa watoto wa kijiji cha Mwamanyiri hulazimika kutembea umbali mrefu kwenda shule ya Igwamanoni, hali inayosababisha baadhi yao kuacha masomo.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso