NA NEEMA NKUMBI- HUHESO DIGITAL KAHAMA
Mkuu mpya wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amemkabidhi rasmi ofisi mkuu mpya wa wilaya ya Kahama, Frank Nkinda, huku akimpa maagizo mazito kuhusu uendelezaji wa maeneo ya kiuchumi, hususan Kongani ya Buzwagi.
Akizungumza katika makabidhiano hayo yaliyofanyika Julai 2, 2025, Mhita ambaye awali alikuwa mkuu wa wilaya ya Kahama, amemtaka Nkinda kuhakikisha anasimamia kikamilifu maendeleo ya kongani hiyo pamoja na maeneo mengine ya uwekezaji ili kulinda uchumi wa wananchi na wa wilaya kwa ujumla.
Mhita amesema:“Baada ya Buzwagi kumaliza shughuli za uchimbaji, serikali iliingia makubaliano na kampuni hiyo kuhakikisha eneo hilo linatumika kama kongani, Mpaka sasa tuna zaidi ya wawekezaji 15, akiwemo Kabanga Nickel, Lengo ni kuhakikisha mzunguko wa fedha unaendelea na wananchi wanainuka kiuchumi. Nenda kasimamie hiyo kongani.”
Ameeleza kuwa kongani ya Buzwagi ni sehemu muhimu ya mkakati wa kuhakikisha wananchi wananufaika moja kwa moja na uwekezaji, kama ilivyoelekezwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.
Katika kuhakikisha mazingira ya uwekezaji yanaimarika, Mhita amesema serikali inaendelea kuboresha miundombinu muhimu kama Bandari Kavu ya Isaka, iliyopo Msalala, ambayo ni kitovu cha usafirishaji wa malighafi kwa wawekezaji.
Akigusia miradi ya maendeleo, Mhita amemuelekeza Nkinda kutumia mapato ya ndani kukamilisha miradi badala ya kungoja fedha kutoka Serikali Kuu.
“Hakuna sababu ya kusema miradi haijakamilika wakati tuna mapato ya ndani, Tunaanzisha miradi mipya ilhali mingine haijakamilika Hii haikubaliki.” Amesisitiza
Kwa upande wake, mkuu mpya wa wilaya Frank Nkinda ameahidi kutekeleza maagizo hayo kwa moyo wa haki, upendo, usawa na kuwahudumia wananchi bila ubaguzi.
Amesema:“Tutaimarisha mshikamano, kuwasikiliza wananchi na kutatua changamoto zao kwa wakati, Naomba ushirikiano wenu.”
Ametoa wito kwa watumishi wa serikali na viongozi wa kisiasa kusimama pamoja kukemea vitendo visivyo vya maadili, hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama, Thomas Myonga, amemtaka mkuu huyo wa wilaya kuendeleza misingi bora ya uongozi iliyowekwa na mtangulizi wake, hususan katika usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Amesema:“Kipaumbele cha wananchi ni maendeleo, Kasimamie utekelezaji wa Ilani, sisi tutakupa ushirikiano, Kahama haina migogoro, tunataka maendeleo.”
Mwisho
No comments:
Post a Comment