SERIKALI YA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN YAENDELEA KUWATAMBUA, KUWATHAMINI NA KUWAHESHIMU WAZEE – RC MACHA - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 14 June 2025

SERIKALI YA MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN YAENDELEA KUWATAMBUA, KUWATHAMINI NA KUWAHESHIMU WAZEE – RC MACHA








#Shinyanga_RS




Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha, amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuwatambua, kuwathamini, kuwaheshimu na kuwatunza wazee wote nchini kwa kutambua mchango wao mkubwa katika ujenzi wa Taifa, kupitia uzoefu, mawazo na maarifa waliyonayo.




RC. Macha ameyasema hayo Juni 14, 2025, wakati akihutubia Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Kuelimisha na Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee Duniani, lililofanyika katika ukumbi CCM Mkoa wa Shinyanga. Kongamano hilo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi za dini, mila, Kamati ya Amani ya Mkoa, Baraza la Jumuiya ya Wazee, pamoja na wananchi.




“Serikali yetu inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuwathamini na kuwatunza wazee wote ili waendelee kufurahia maisha kama walivyo wananchi wengine. Wazee ni kundi muhimu, na ndio maana Serikali imeendelea kuhakikisha wanapatiwa kipaumbele katika huduma za kijamii, ikiwemo kuanzisha madirisha maalum ya kuwahudumia wanapofika katika vituo vya kutolea huduma za afya,” alisema RC Macha.




Kwa niaba ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bi. Felister Mndem, aliwasilisha salamu rasmi, akisisitiza umuhimu wa kuendeleza malezi bora kwa wazee kwa kuwajengea moyo wa huruma, heshima kwa wazee, na ushiriki katika shughuli za kuwatunza wazee katika jamii.




“Wazee siyo mzigo bali ni hazina yenye thamani kwa Taifa letu. Tunapaswa kuwakuza vijana wetu katika misingi ya maadili mema, utu na mshikamano ili kujenga jamii yenye heshima kwa wazee na kuheshimu mchango wao,” alisema Bi. Mndem.


Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, Mkoa wa Shinyanga ulikuwa na watu 100,626 wenye umri wa miaka 60 na kuendelea, sawa na asilimia 4.5 ya watu wote katika Mkoa huo, ambao walifikia 2,241,299. Kwa mwaka 2025, idadi hiyo inakadiriwa kuongezeka hadi 101,114 kati ya watu 2,483,928, sawa na asilimia 4.1.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso