WAANDISHI WA HABARI WASHUHUDIA HATUA ZA MAENDELEO JIJINI MWANZA KUPITIA MIRADI YA KIMKAKATI YA SERIKALI - HUHESO DIGITAL BLOG

Breaking

Post Top Ad

Saturday, 3 May 2025

WAANDISHI WA HABARI WASHUHUDIA HATUA ZA MAENDELEO JIJINI MWANZA KUPITIA MIRADI YA KIMKAKATI YA SERIKALI


NA NEEMA NKUMBI- HUHESO DIGITAL MWANZA


Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli na ya haraka kupitia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, hususan katika ukanda wa Ziwa Victoria.


Waandishi wa habari kutoka mikoa ya Mwanza na Shinyanga wamepata fursa ya kutembelea miradi hiyo muhimu inayotekelezwa na Serikali katika Jiji la Mwanza Mei 2, 2025, katika ziara iliyoandaliwa na Ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali.

Ziara hiyo imeongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa.


Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa vivuko vipya vitano, ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi, pamoja na meli kubwa ya kisasa ya MV Mwanza ambayo imekamilika kwa asilimia 98 ambapo Miradi hii inalenga kuondoa changamoto sugu za usafiri na usafirishaji, kukuza biashara, na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Ziwa Victoria na nchi jirani.




Akizungumza na waandishi wa habari katika ziara hiyo, Bw. Msigwa ameeleza kuwa miradi hiyo ni alama ya mafanikio makubwa yanayopatikana kupitia utekelezaji wa dira ya maendeleo ya Serikali ya Awamu ya Sita.




“Miradi hii ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali kuleta maendeleo ya kweli na ya haraka kwa wananchi Tunataka wananchi wote wajue kinachoendelea na wawe sehemu ya mafanikio haya,” alisema Msigwa.




Katika ziara hiyo, waandishi walipata nafasi ya kujionea maendeleo ya miradi, kuuliza maswali kwa wahandisi na wakandarasi, na kushuhudia kwa karibu usimamizi wa Serikali katika kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora unaotakiwa na ndani ya muda uliopangwa.




Daraja la Kigongo – Busisi, ambalo linatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa wakazi wa Wilaya ya Misungwi na Sengerema, limekamilika kwa asilimia 99 na linatarajiwa kufunguliwa rasmi wakati wowote na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo Daraja hilo, linalogharimu zaidi ya shilingi bilioni 700, litakuwa kiungo muhimu si tu kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa bali pia kwa nchi jirani, hivyo kuimarisha biashara ya kikanda.




Mbali na hilo, Bw. Msigwa ameeleza kuwa Serikali imekarabati vivuko saba vya usafirishaji wa watu na mizigo katika Ziwa Victoria, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuboresha miundombinu na kuinua uchumi wa wananchi.




Ziara hiyo imeleta picha halisi ya namna Serikali ya Awamu ya Sita inavyotekeleza kwa vitendo miradi ya maendeleo kwa uwazi na kwa kushirikisha umma, Kasi ya ujenzi wa miundombinu bora inatoa matumaini makubwa kwa Watanzania, huku Serikali ikionesha mfano wa kuigwa barani Afrika katika kuweka kipaumbele kwa huduma za kijamii, uchumi jumuishi, na mshikamano wa kitaifa.




Mwisho.




No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Pages

Huheso